Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP wajitosa kuisaidia Lebanon kwani bila bandari ya Beirut, hali itakuwa mbaya zaidi Lebanon  

WFP wajitosa kuisaidia Lebanon kwani bila bandari ya Beirut, hali itakuwa mbaya zaidi Lebanon  

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya pili tangu kutokea kwa mlipuko mkubwa katika bandari mjini Beirut, nchini Lebanon, shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP limesema linafanya tathimini ya haraka ili kujiweka tayari kutoa msaada wa dharura kwa maelfu ya watu ambao wamejikuta katika hali ya kukosa makazi, wamejeruhiwa na pia wamewapoteza wapendwa wao. Jason Nyakundi na maelezo zaidi 

Bandari ya Beirut na sehemu kubwa ya mji huo imeachwa na magofu na vilio vya kila namna. WFP inasema Lebanon hata kabla ya tukio hilo la kusikitisha, ilikuwa tayari katika hali mbaya ya uchumi kuwahi kutokea katika historia yake na hali hiyo ilikuwa inafanywa kuwa mbaya zaidi na janga la COVID-19

Uharibifu mkubwa uliosababishwa na mlipuko huo katika bandari hii kubwa zaidi nchini Lebanon, kutapaisha zaidi bei ya vyakula kufikia kiwango ambacho si wengi wataweza kukimudu kwani nchi hiyo inaagiza chakula chake kutoka nje kwa asilimia 85 na kwa kiasi kikubwa kinapokelewa katika bandari ya Beirut. 

Kapteni Joinal Abedin kutoka kikosi kazi cha majini, MTF cha ujumbe wa kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL ambao moja ya meli yao imeharibiwa na baadhi ya maafisa wake kujeruhiwa, anaeleza alivyoshuhudia tukio hilo,  

 “Ilikuwa siku ya kawaida, kila mtu alikuwa anafanya kazi yake na watu walikuwa wanazunguka hap ana pale wakitekeleza majukumu yao na ghafla tukaona kuna moto mdogo. Kwa hivyo moto mdogo haimaanishi kutakuwa na uharibifu. Baada ya dakika mbili moto ukaja karibu na tulikuwa bado tunaona ni kawaida kisha ghafula kukawa na mlipuko mkubwa ambao ulitokea ndani ya sekunde chache. Sijui namna mlipuko wa Hiroshima ulivyokuwa, lakini ulikuwa karibu sawa na huo.” 

Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa ukaribu na mamlaka za Lebanon ili kusaidia kukabiliana na matokeo ya mlipuko huo mkubwa ambao umetokea huku raia milioni moja wa Lebanon wakiishi chini ya mstari wa umasikini yaani chini ya dola moja kwa siku. 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Jason Nyakundi
Audio Duration
1'48"