Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yachukua hatua mtambuka kunusuru watoto dhidi ya unyafuzi

UNICEF yachukua hatua mtambuka kunusuru watoto dhidi ya unyafuzi

Pakua

Nchini Niger, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linashirikiana na wadau kutekeleza mbinu za haraka za kukabiliana na utapiamlo uliokithiri miongoni mwa watoto pamoja na mbinu endelevu za muda mrefu kuepusha watoto kutumbukia kwenye utapiamlo. John Kibego na ripoti kamili. 

Safari yetu ya kubaini hatua za UNICEF kukabili unyafuzi na utapiamlo katika mikoa ya Maradi na Zinder nchini Niger ambako watoto takribani 200,000 hutibiwa dhidi ya hali hiyo, inatukutanisha na Souley Adam, mtaalamu wa lishe wa UNICEF akihusika na maeneo hayo. 

Souley anasema kuwa kila uchao hutembelea jamii kwenye eneo hilo na kwa kutambua kuwa kinga ni bora kuliko tiba, wameunda vikundi vya kuelimisha wanawake kukabili utapiamlo na wanafundishwa mapishi ya mlo bora. 

“Leo asubuhi wanawake wamekusanyika kujifunza mapishi. Utapiamlo hausababishwi na ukosefu wa lishe ya kutosha pekee, bali pia na ulaji wa hovyo. Kumlisha mtoto chakula bora na cha kutosha ni muhimu, lakini pia usafi ni muhimu na ndio maana tunaelimisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi. Na kuwarahisishia kupata maji safi na salama na pia vyoo.” 

Wanawake wanaelimishwa dalili za utapiamlo, kwa kuwa ukitibiwa mapema hata kasi ya kupona ni kubwa, na kwa wale walio na unyafuzi, wamelazwa hospitali na Souley amewatembelea  

“Hali za watoto ni tete, na baadhi yao hubakia na ulemavu wa kudumu. Namfahamu mtoto mmoja wa kike ambaye aliugua utapiamlo na sasa hawezi tena kutembea. Na ndio maana tunahaha kusaidia hawa watoto hata katika safari yao ya kupona.” 

UNICEF inahakikisha kuwa watoto walioko hospitali pamoja na matibabu ya dawa wanafanyiwa pia mazoezi ya viungo na msaada wa kisaikolojia ili kuhakikisha maendeleo yao ya kujitambua na pia ubongo. 

Audio Credit
Assumpta Massoi\John Kibego
Audio Duration
1'48"
Photo Credit
UNICEF VIDEO