Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lebanon yaomboleza, UNIFIL iko tayari kusaidia

Lebanon yaomboleza, UNIFIL iko tayari kusaidia

Pakua

Nchini Lebanon, taifa hilo la Mashariki ya Kati liko katika siku ya maombolezo kufuatia mlipuko mkubwa wa jana katika mji mkuu Beirut uliosababisha vifo vya watu wapatao 100 huku zaidi ya 4000 wakijeruhiwa. 

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo kupitia ukurasa wake wa Twitter ameonyesha masikitiko yake akirejelea salamu zake za rambirambi alizotoa jana kwa familia za wafiwa na huku akitakia majeruhi ahueni ya haraka. 
Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limeeleza mshtuko wake kufuatia mlipuko huo mjini Beirut, likitiwa wasiwasi na ustawi wa watoto sambamba na kusadia wadau wake mjini humo kwa msaada wowote utakaohitajika. 

Wakati huo huo, msemaji wa ujumbe wa kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, Andrea Tenenti amesema kuwa pamoja na jukumu lao la kusimamia eneo la mpakani kwa Isreali na Lebanon lisilo na mapigano,  
“Kama kamanda wa kikosi alivyosema jana, hivi sasa tunashikamana na watu na serikali ya Lebanon, na tuko tayari kusaidia na kutoa msaada wowote ambao utazingatia mahitaji yao. Mlipuko ulikuwa mkubwa sana eneo la chini zaidi mjini Beirut limeharibiwa na maeneo mengine pia ya mjini vivyo hivyo. Kwa hiyo bado tunajaribu kutathmni hali ilivyo ikiwemo kiwango cha uharibifu kwa wanajeshi wetu.” 
Hapo jana UNIFIL katika taarifa yake ilisema kuwa a kuwa walinda amani kadhaa wamejeruhiwa. 
Kwa mujibu wa UNIFIL, mlipuko huo umesababisha majeraha makubwa kwa wafanyakazi wanane wa kikosi kazi cha majini, MTF, na majeruhi kidogo kwa wengine kadhaa. 
Majeruhi wote hao ni walinda amani kutoka Bangladesh na walikuwa katika jukumu ndani ya meli iliyokuwa imetia nanga bandarini Beirut. 

 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'35"
Photo Credit
Pasqual Gorriz/UNIFIL