Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kama maambukizi ya COVID-19 ndani ya jamii yamedhibitiwa, fungueni shule – Guterres

Kama maambukizi ya COVID-19 ndani ya jamii yamedhibitiwa, fungueni shule – Guterres

Pakua

Janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 likiendelea kuripotiwa maeneo mbalimbali duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa tamko lake la kisera lenye mambo makuu manne ya kuzingatia ili kuhakikisha kuwa janga hilo halizidishi pengo lililokuwa la walio na elimu na wasio na elimu. Flora Nducha na ripoti kamili. 

Tamko hilo alilolitoa kwa njia ya video jijini New York, Marekani hii leo pamoja na kuweka bayana changamoto za elimu zilizokuwepo kabla ya Corona na baada ya Corona, linaeleza kuwa hata hatua zilizochukuliwa za kutoa elimu kwa njia ya televisheni na radio wakati huu ambapo shule zimefungwa bado zimeonesha pengo la wenye fursa na wasio na fursa. 

“Licha ya masomo kupelekwa kwa njia ya redio, televisheni na mtandaoni, na juhudi kubwa za walimu na wazazi, wanafunzi wengi bado hawajafikiwa. Wanafunzi wenye ulemavu, wale walio katika jamii ndogo au za pembezoni, wakimbizi wa ndani, wakimbizi na wale walio maeneo ya ndani wako hatarini kuachwa nyuma.” 

Amesema hata wale wanaobahatika kupata elimu kwa njia hizo bado mafanikio yanategemea mazingira wanamoishi ikiwemo mgawanyo sawia wa majukumu ya nyumbani na ni kwa mantiki hiyo tamko lake la kisera linazindua kampeni mpya ya Umoja wa Mataifa na wadau wa elimu ikipatiwa jina Okoa Mustakabali wetu. 

Mosi, fungueni shule. Pindi maambukizi ya COVID-19 ndani ya jamii yakidibitiwa kurejesha watoto shule na vyuoni kwa usalama iwezekanavyo lazima kiwe kipaumbele. Tumetoa mwongozo kwa serikali kutekeleza suala hilo gumu. Pili, kupatia kipaumbele elimu wakati wa maamuzi ya kifedha, tatu kulenga wanafunzi walio mbali kufikiwa nan ne mustakabali wa elimu uko hapa. Tuna fursa ya kizazi ya kuangalia upya elimu. Dunia inapokabiliwa na ukosefu wa usawa katika viwango tunahitaji elimu- kitu cha kujenga usawa kuliko wakati wowote ule.” 

Katibu Mkuu amesema ni lazima kuchukua hatua za kijasiri hivi sasa ili kujenga jamii jumuishi, yenye mnepo, mifumo yenye elimu bora kwa itakayoendana na siku za zijazo.” 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Flora Nducha
Sauti
2'14"
Photo Credit
© UNICEF/Frank Dejongh