Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliobakwa DRC wana machungu kiasi cha kushindwa kusimulia ili wasaidiwe

Waliobakwa DRC wana machungu kiasi cha kushindwa kusimulia ili wasaidiwe

Pakua

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC matukio ya ukatili wa kingono ikiwemo ubakaji yanaendelea kutekelezwa kimfumo na vikundi vinavyopigana kwenye taifa hilo lililoshuhudia mapigano mara kwa mara. Flora Nducha na ripoti kamili. 

Mjini Bunia, jimboni Ituri nchini DR Congo, katika ofisi za shirika la kiraia la SOFEPADI, linalosaidia wanawake na watoto waliokumbwa na ukatili wa kingono na ubakaji. 

Matukio ya ubakaji yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara kupitia ripoti za Umoja wa Mataifa yakitajwa kuwa ni uhalifu siyo tu kwa mujibu wa sheria za DRC bali pia sheria za kimataifa. 

Élisabeth Furaha, ni daktarin kwenye kliniki ya SOFEPADI na anasema kuwa,  "sisi ndio tunaokutana na waathiriwa wa ukatili wa kingono kwa mara ya kwanza tu baada ya tukio. Kwa mwezi Januari pekee, tumepokea waathirika 46 wa ukatili wa kingono tumewapatia dawa za virusi vya UKIMWI, vidonge vya kuzuia mimba zisizotakiwa. Wanapata pia kipimo cha kujua iwapo wamepata ujauzito au la na pia vipimo vya UKIMWI.” 

Kwa Noëlla Alifwa ambaye ni mmoja wa waasisi wa SOFEPADI hali wanayoiona inakuwa si nzuri kwa kuwa,  "watu wanaofika hapa wamebakwa, wameteswa, wamejeruhiwa. Na kile ambacho ni kigumu kwetu ni kwamba hivi karibuni tumeona watoto ambao wameuawa.” 

Manusura wanawake na watoto, kutokana na machungu waliyopitia inakuwa vigumu sana kusimulia yaliyowakumba na hata kutaja jina, hivyo SOFEPAD imeajiri mwanasaikolojia.  

 Miongoni mwa wateja wa leo ni mwanamke mmoja anayefanya kazi mashambani ambaye yeye na binti yake walibakwa, na sasa kwa pamoja wanamlea mtoto aliyezaliwa kutokana na kitendo hicho. 

Gloria Malolo anafanya kazi na ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na DRC yenye mamlaka ya kusaka haki na fidia kwa waathirika wa ubakaji na wanafanya kazi kwa ushirikiano na kliniki ya SOFEPADI.  Gloria anasema kwamba, "tunaweka kumbukumbu ya hizo kesi  ili tuweze kuziwasilisha kwenye mfumo wa sheria, hasa ule wa kijeshi, kwa kuwa wao wana uwezo wa kuamua kuhusu makosa yaliyofanywa na vikundi vilivyojihami au jeshi la serikali. Baada ya hapo wanawajibika, kama mamlaka, kuweka kumbukumbu na kuchunguza ukiukwaji huu wa haki za binadamu.  

Audio Credit
Anold Kayanda/ Flora Nducha
Audio Duration
2'24"
Photo Credit
MONUSCO