Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yasaidia wana Kasese kukabili madhila ya mafuriko

UNICEF yasaidia wana Kasese kukabili madhila ya mafuriko

Pakua

Kutokana na mafuriko ya kila mwaka yanayoikumba wilaya ya Kasese nchini Uganda, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kushirikiana na serikali ya Uganda, wanaendelea kuimarisha mifumo ya kuhakikisha kunakuwa na mazingira ya kuchukua hatua za haraka kunapokuwa na dharura kama hizo. John Kibego na maelezo zaidi. 

Kila mwaka wilayani Kasese, mafuriko yanapasua katika bonde na kutengeneza njia ya uharibifu, kufukia nyumba za watu,ardhi na njia zao nyingine za maisha kisha kuwaacha wengi wakiwa wametawanywa bila  chakula, malazi na usalama. Elizabeth Kabugo ambaye sasa anajihifadhi yeye na mwanaye mchanga kwenye hema alilopewa na UNICEF anasema, “awali tulifikiri tutakuwa nyumbani kufikia mwezi huu wa Julai lakini sasa kwa mvua zaidi hizi na mafuriko, hilo linaonekana haliwezekani.Tumebaki tu tunashangaa kama mafuriko yatafika wakati yaishe.”  

Mafuriko haya si tu yamevamia makazi ya watu, hata shule hazikubaki salama. Anatory Nyamanbisi ni mwalimu katika shule ya msingi ya Kisabu anasema, "maji yalikuja kutoka mlimani yakafagia kila kitu na yakafika katikati ya madirisha. Madarasa yetu matatu yalivinjika. Kila kitu kilisombwa.Kimsingi tulikuwa na mshituko.  

UNICEF kwa kushirikiana na serikali ya Uganda, wanaendelea kuimarisha mifumo, kuhakikisha hatua za haraka katika hali ya dharura na kuzuia magonjwa yatokanayo na maji machafu kama vile kipindupindu kwa kuwafikia watu walioko hatarini na huduma za kuokoa maisha. Susan Birungi Nyankoojo ni afisa wa masuala ya dharura wa UNICEF.

Afisa huyo anasema kuwa, "wilaya ya Kasese ni moja ya maeneo yetu muhimu na tunahakikisha tunaimarisha mifumo na kuhakikisha tunaziwezesha jamii, kuwawezesha kujenga mnepo, ni kipaumbele kwetu sisi UNICEF.” 

Audio Credit
Anold Kayanda/John Kibego
Audio Duration
1'53"
Photo Credit
Arne Hoel/World Bank