Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipochukua hatua sahihi na kwa haraka, Amerika Kusini na Karibea watu watakufa- WFP

Tusipochukua hatua sahihi na kwa haraka, Amerika Kusini na Karibea watu watakufa- WFP

Pakua

Shirika la Mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limeonya kuwa kuongezeka kwa njaa, uchumi unaoyumba, ukosefu wa usawa na msimu wa vimbunga vikali, vinatishia watu wa Amerika Kusini na Karibea na vinaweza kuwa na athari zaidi kama hatua za haraka hazitachukuliwa

Katika mji Mkuu wa Peru, kwa wahamiaji wengi kutoka Venezuela, kusafisha vioo vya magari yanayosimama katika taa za barabarani, ni njia pekee ya kuufanya mkono uende kinywani. Wengi wao walipoteza kazi zao kutokana na janga la COVID-19. Inakadiriwa kuwa takribani wavenezuela 31,000 wamerejea kwa miguu katika nchi yao ya asili kutokana na janga hili la virusi vya corona. Raúl Montero ni mhamiaji kutoka Venezuela anasema,"nilipoteza kazi yangu kwasababu ya janga la corona. Na sasa ninalazimika kusafisha vioo vya magari. Sikuwahi kufanya kazi hii awali lakini ili kupeleka chakula nyumbani kwa ajili ya watoto, ninalazimika kuifanya.” 

Maambukizi ya virusi vya corona yakiongezeka, Amerika ya Kusini imekuwa eneo lililoathirika zaidi likiwa na zaidi ya robo ya wagonjwa wote duniani. Kwa mujibu wa WFP, Amerika Kusini na Karibea wanategemea kushuhudia ongezeko la asilimia 269 ya idadi ya watu wanaokabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na hivyo kufikia jumla ya watu milioni 16 ambao hawajui ni wapi mlo wao unaofuata utakotoka katika miezi ijayo. Hiyo ni ongezeko la watu milioni 4.3 ikilinganishwa na mwaka jana 2019. Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, David Beasley akiwa Ibarra, jimbo la Imbabura nchini Ecuador anasema,“ni mchanganyiko mbaya sana na tunatakiwa kuchukua hatua sasa na tunapaswa kuwa werevu. Huwezi kushugulika tu na COVID-19 au njaa peke yake. Vinatakiwa kushughulikiwa kwa pamoja. Ikiwa tutafanya sawasawa  tunaweza kuokoa maisha. Tusipofanya kwa usahihi, watu watakufa.” 

 WFP ina wasiwasi hususani kwa watu walioko hatarini nchini Haiti, ushoroba mkavu wa Amerika ya kati na pia wahamiaji raia wa Venezuela walioko Colombia, Ecuador na Peru.

WFP inatoa mgao wa chakula cha kupeleka nyumbani kwa ajili ya watoto ambao hawawezi tena kuhudhuria shuleni, vocha na fedha taslimu pia ili watu waweze kununua katika maduka karibu nao. Nchini Honduras pekee, WFP imetoa mgao wa dharura kw familia 29,000 zilizoathiriwa na janga la COVID-19.  

 

Audio Credit
Assumpta Massoi\John Kibego
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
WFP/Guillermo Galdos