Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto waanza kuona nuru kusini mwa Madagascar

Watoto waanza kuona nuru kusini mwa Madagascar

Pakua

Msaada uliotolewa na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na serikali ya Norway umewezesha watoto katika maeneo ya kusini mwa Madagascar kuweza kupata elimu katika mazingira yenye staha. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Maeneo hayo ni wilaya za Anosy, Androy na Atsimo Andrefana ambako hali ya maisha ni duni ambapo msaada huo uliotolewa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 umezaa matunda.

Serikali ya Norway ilitoa dola milioni 21 za kutekeleza mradi huo wa msaada uliokuwa katika maeneo matatu, ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF lilipatia mafunzo walimu 11,364 sambamba na vifaa vya kufundishia kwa shule 4,000.

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP lenyewe lilihusika na ujenzi wa majengo 350 ya kantini katika shule 70,520 huku shirika la kazi duniani, ILO likijenga vyumba 158 vya madarasa na ukumbi wa kulia chakula katika shule 97.

Mkurugenzi wa elimu ya msingi katika kituo cha Amphany nchini Madagascar Emilie Tamara anasema kuwa, “katika nchi yetu, kiwango cha watoto kumakinika kinaongezeka. Wale ambao walikuwa watoro shuleni sasa wamerejea, hii ni kwa sababu ya mbinu bora za kufundishia. Walimu na wafanyakazi wengine wa shule wamepatiwa mafunzo ya kina. Shule yetu pia imepata majengo mapya, madawati mapya vifaa vipya vya kufundishia, na pia tuna kantini ya shule ambayo ni kivutio pia kwa watoto kufika shuleni.”

Mkurugenzi huyo wa elimu ya msingi anaenda mbali kusema kuwa kiwango cha ufaulu kwenye mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kimepanda kutoka asilimia 64 mwaka 2017 hadi asilimia 98 mwaka 2019.

Halikadhalika kiwango cha kurudia elimu ya msingi kwenye maeneo hayo kimeshuka na kufikia asilimia 26 ikiwa ni chini ya wastani wa kiwango cha kitaifa cha asilimia 28.4.

Akizungumzia msaada wao, Afisa kwenye ubalozi wa Norway kwenye mji mkuu wa Madagascar, Antananarivo,  Andreas Danevad amesema kuwa, “elimu ni moja ya vipaumbele vikuu vya Norway kwenye ushirikiano wa kimataifa. Inafikia karibu theluthi mbili ya ushirikiano wetu wa kimaendeleo na Madagascar. Tunafurahia sana kuweza kuendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa ili hatimaye Madagascar iweze kufanikisha lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ambalo ni elimu bora.”

 

Audio Credit
Anold Kayanda/Assumpta Massoi
Sauti
2'51"
Photo Credit
© UNICEF/UNI302583/Ralaivita