Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za kupambana na COVID-19 zazidisha machungu kwa wayemen

Harakati za kupambana na COVID-19 zazidisha machungu kwa wayemen

Pakua

Nchini Yemen, vita vya wenyewe kwa wenyewe na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, vimeleta taabu kwa wananchi huku familia zikihaha kujinusuru na Umoja wa Mataifa ukiingilia kati kusaidia. Assumpta Massoi anaarifu zaidi.

Hali si shwari nchini Yemen ambako hali ya upatikanaji wa afuta nao si mzuri, madereva katika mji mkuu, Sana’aa wakikesha kusubiri kununua mafuta na hata wakati mwingine baada ya kusubiri muda mrefu mafuta kumalizika kituoni.

Adha hizi si jambo geni kwa Saeed, Ahmed, mwenye umri wa miaka 61 ambaye awali alikuwa anajipatia kipato kwa kuuza chakula cha kijadi cha Yemen kiitwacho Sahawiq.

Hata hivyo maisha yalibadilika wakati wa vita baada ya kombora kutoka angani kutua kwenye eneo lao na kumsababishia ulemavu, ambapo sasa anapata fedha kwa kuchunga kondoo, fedha ambazo hazimtoshelezi yeye na familia yake ya watoto 13, wawili kati yao wakiwa wana ulemavu.

Saeed anasema kuwa, “nina mabinti wawili ambao wana ulemavu. Natumia fedha nyingi kuwapatia tiba na niliwapeleka mjini Sana’a baada ya chama kimoja kunisaidia. Kila mmoja alifanyiwa upasuaji mara tatu. Nilikopa fedha za dawa zao na nikauza dhahabu ya mama yao kwa ajili yao. Binti yangu huyu alifanyiwa upasuaji wa ubongo. Nilikaa naye miezi miwili mjini Sana’a ili aweze kupata dawa sahihi. Niliacha familia yangu peke yao.”

Wanawake wakiwa wamepanga foleni kwenye kituo cha mgao kambini Kharaz nchini Yemen, ambako pia hatua za kukabiliana na Corona zinazingatiwa.
© UNOCHA/Mahmoud Fadel
Wanawake wakiwa wamepanga foleni kwenye kituo cha mgao kambini Kharaz nchini Yemen, ambako pia hatua za kukabiliana na Corona zinazingatiwa.

Hata hivyo mgao wa vocha za chakula kutoka shirika la mpango wa chakula la Umoja wa  Mataifa, WFP, umekuwa msaada mkubwa kwa Saeed ambapo anaweza kwenda dukani na kupatiwa unga, kunde, mafuta, sukari na chumvi.

Kwa upande wa kukabiliana na COVID-19, mwezi Juni mwaka huu, WFP iliwasilisha kwa ndege shehena ya tani 43 za vifaa vya maabara, mashine za kusaidia kupumua, vifaa vya kupima Corona, na mavazi ya kujikinga au PPE.

Tathmini ya WFP kwa watu milioni 7.9 kwenye wilaya 133 za Yemen zilizochunguzwa, ilibaini kuwa milioni 2 walikuwav wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kati ya mwezi Februari na Aprili mwaka huu, idadi hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 25 ya waliochunguzwa.

Halikadhalika utafiti unakadiria kuwa kati ya mwezi huu wa Julai na Desemba mwaka huu, idadi ya watu watakaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula itaongezeka na kufikia milioni 3.2, ingawa WFP inasema kuwa, kiwango hicho kimepungua ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018/2019.

Ukosefu wa chakula Yemen unasababishwa na mapigano yanayoendelea ambayo hufanya wasambazaji wa misaada ya binadamu ikiwemo chakula washindwe kufikia wahitaji. Halikadhalika masoko kufungwa na watu kukimbia makazi yao.

Majimbo yaliyoathirika zaidi ni Taizz, Lahj na Hadramaut.

 

 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta Massoi
Audio Duration
2'49"
Photo Credit
© UNICEF