Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF inasema, ebola imeongeza idadi ya watoto waliotenganishwa na wazazi DRC

UNICEF inasema, ebola imeongeza idadi ya watoto waliotenganishwa na wazazi DRC

Pakua

Watoto zaidi ya 32 wamepoteza au kutenganishwa na mzazi mmoja au wote kutokana na Ebola tangu kuzuka kwa mlipuko mpya Juni Mosi kwenye jimbo la Equateur Magharibi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC,limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Kinshasa shirika hilo limeonya kwamba hatua za haraka zinahitajika kuongezwa sasa kabla hali hiyo haijageuka kubwa janga kubwa.

Mlipuko wa Ebola uliopita 2018 jimboni Equateur ulidhibitiwa ndani ya miezi miwili kutokana na kasi na kiwango cha hatua zilizochokuliwa na msaada wa wahisani.

Hatahivyo UNICEF imesema hivi sasa bado haijapokea fedha zozote za kupambana na mlipuko huu mpya.

Likishirikiana na wadau shirika hilo limeshawasaidia watoto 10 na kuwaweka katika vituo vya muda vya ulinzi wakati mzazi mmoja au wote wakifanyiwa vipimo au kupewa matibabu katika moja ya vituo vinne vya matibabu ya ebola jimboni humo.

UNICEF imesisitiza kwamba kwa sasa inahitaji msaada wa haraka ili iweze kujenga vituo vya kuhifadhi watoto hao karibu na vituo vya matibabu ya Ebola ili kuweza kutoa huduma inayostahili kwa watoto waliotenganishwa na wazazi wao.

Edouard Beigbeder mwakilishi wa UNICEF nchini DRC amesema, “kama tulivyoshuhudia katika milipuko iliyopita Ebola inaathiri watoto kwa njia nyingi zaidi ya hatari ya muda mfupi ya maambukizi na vifo. Iwe watoto wenyewe wameambukizwa au kuona wazazi au wanafamilia wengine wakiambukizwa, wanahitaji huduma maalum na msaada wa kisaikolojia na kimwili. Tunapaswa kufanya kila kitu kupunguza athari za mlipuko huu kwa ustawi wa watoto.”

Huu ni mlipuko wa 11 wa Ebola nchini DRC tangu mwaka 1976 na hadi sasa jimboni Equauter umeshaambukiza watu 62 na vifo 27 vikiwemo vya watoto wawili na takwimu za UNICEF zinaonyesha kwamba watoto wa umri wa kati ya miaka 2 na 17 wamepitia moja ya milipuko hiyo minne ya Ebola.

UNICEF inahitaji dola milioni 6.98 kwa ajili ya shughuli zake za kupambana na Ebola jimboni Equateur na ilichonacho hadi sasa ni dola milioni 2 tu kutoka kwenye hazina yake ili kukidhi mahitaji ya muhimu hadi ufadhili utakapopatikana.

Audio Credit
Flora Nducha/Hilda Phoya
Audio Duration
2'11"
Photo Credit
UN /Martine Perret)