Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya FAO yaonesha dunia imepoteza ekari milioni 178 za misitu tangu 1990

Ripoti ya FAO yaonesha dunia imepoteza ekari milioni 178 za misitu tangu 1990

Pakua

Ripoti mpya ya tathimini ya rasilimali ya misitu iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kilimo na chakula FAO imesema upotevu wa misitu duniani bado unaendelea ingawa sio kwa kiwango kikubwa sana. Jason Nyakundi anaarifu zaidi.

Ripoti hiyo mpya ya aina yake iliyozinduliwa leo mjini Roma Italia kwa mujibu wa FAO ni ya kina na imemulika zaidi ya vyanzo 60 vya upotevu wa misitu kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1990 hadi 2020.

Annsi Pekkarinen afisa misitu wa FAO amesema ujumbe muhimu wa ripoti hiyo ni kwamba, “misitu inaendelea kupotea ingawa kidogo si kwa kasi kikubwa sana kama ya awali ingawa upunguaji huo hautoshi, kwani dunia imepoteza tayari ekari milioni 178 za misitu tangu 1990, ekari ambazo ni sawa na ukubwa wa nchi nzima ya Libya ukizingatia kwamba duniani kote kuna jumla ya ekari bilioni 4.08 za misitu.”

Ameongeza kwamba ingawa upotevu wa misitu unaendelea kila kona ya dunia kitovu ni Afrika, ikifuatiwa na Amerika ya Kusini.

Ripoti hiyo imesema tangu mwaka 1990 ekari zingine milioni 420 za misitu zimepotea kutokana na matumizi mengine ambayo si ukataji miti kwa ajili ya mbao bali ni kwa ajili ya kilimo, huku Afrika eneo kubwa la misitu hiyo inayopotea likitumika kwa ajili ya upanuzi wa makazi kutokana na ongezeko la watu.

Hata hivyo ripoti imesema bado kuna mipango muhimu ya kuilinda misitu hiyo ambapo asilimia 18 ya misitu yote duniani imewekewa mikakati maalumu ya kuwa endelevu na kuilinda.

Kwa mujibu wa FAO takwimu za tathimini hiyo zimekusanywa kutoka nchi 236 na sasa zimewekwa katika mfumo maalum wa kidijitali ambao pia umezinduliwa na mfumo rahisi wa kuziwezesha upatikanaji wa takwimu hizo.

 

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
5'49"
Photo Credit
FAO/Rudolf Hahn