Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na wadau wanusuru watoto na unyafuzi Madagascar

UNICEF na wadau wanusuru watoto na unyafuzi Madagascar

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linashirikiana na serikali ya Madagascar ili kunusuru watoto waliokumbwa na utapiamlo uliokithiri ambao umesababishwa na ukame wa muda mrefu kusini kwa taifa hilo. John Kibego na maelezo zaidi.

Kutana na Sambezaffe, mama wa watoto 10 mkazi wa eneo la kusini mwa Madagascar akimtambulisha mwanae Sarah Volafeno mwenye umri wa miezi 10.Mwanae huyo ni miongoni mwa watoto milioni 2.5 nchini Madagascar wanaokabiliwa na utapiamlo uliokithiri au unyafuzi. Sambezaffe anasema kuwa,“Watoto wangu wote 10 walipata unyafuzi. Kila mwaka hatuna chakula cha kutosha kulisha familia. Uhaba wa chakula ndio sehemu ya maisha yetu.”

Kutokana na hali hii, UNICEF kwa msaada wa fedha kutoka serikali ya Japan, ikatekeleza miradi kadhaa ya kuimarisha lishe kwa familia kama anavyoelezea Sougrah Myriam Issa, afisa wa kituo cha afya. “Tunashirikiana na mawakala wa jamii ili kusimamia masuala ya lishe kwa wananchi. Tunafundisha wazazi jinsi ya kubaini watoto wao wenye unyafuzi, na wakibainika wanaelekezwa haraka kwenye kituo cha karibu cha afya au hospitali. Pia tunatumia kliniki za kwenye magari kufikia jamii zilizo maeneo ya ndani zaidi, mfano kilometa 10 kutoka kituo chetu cha afya.”

Kwa kuwa uhaba wa maji pia ni sababu ya unyafuzi, UNICEF inahakikisha kuwa familia zinapata maji safi na salama kutoka vituo vya afya.Sambezaffe anasema,“Kupata huduma za afya, kunatupatia maisha bora kwa kuwa tunanufaika na mipango hiyo.”Japan tangu mwaka 2016 imekuwa inatekeleza mpango wa chakula na lishe kwa nchi za Afrika, IFNA.

Audio Credit
Flora Nducha/John kibego
Sauti
1'44"
Photo Credit
© UNICEF/UNI302583/Ralaivita