Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunashukuru Restless Development imetusaidia kujitambua vijana

Tunashukuru Restless Development imetusaidia kujitambua vijana

Pakua

Miongoni mwa wasichana waliosaidiwa na Restless Development na kuweza kuelewa kuhusu masuala ya afya ya uzazi na hivyo kujikinga ni Amina Mahia mkazi wa Dodoma.

Amina anasema kuwa, "kabla sijaingia katika mradi nilikuwa nafikiri kwamba afya ya uzazi ni kuhusiana tu na mfumo mzima wa afya lakini kumbe afya ya uzazi  ni ile hali ya kuwa sawa kimwili, kiakili na kijamii na afya nzima kwa ujumla. Kama vile uzazi wa mpango, mimba za utotoni, usawa wa kijinsia, ukeketaji na mila potofu zote ambazo ziko katika jamii zetu. Kitu kikubwa ambacho kimeninufaisha ni kwamba nimeweza kujitambua kwamba mimi ni nani na hivyo kuleta mchango mkubwa sana katika maisha yangu kwenye suala zima la kuelewa afya ya uzazi."

Judithi Kitinga ni Mratibu Msaidizi wa mradi wa Vijana Tunaweza ulioko chini ya Restless Development mkoani Dodoma nchini Tanzania ana anaelezea changamoto katika kusongesha malengo yao. 

Judith anasema kuwa, "Hili suala la elimu ya afya ya uzazi linagusa tarkibani malengo yote ya maendeleo. Unafaamu binti au kijana akishakuwa na ule uelewa akawa na ile elimu, atatambua ni namna gani yeye mwenyewe ajitunze mwili wake. Na mwili kama tunavyoelewa, usipokuwa na magonjwa, ukijitunza vizuri ndipo unapokuwa na uwezo mzuri wewe wa kufanya kazi mbalimbali na kushiriki kwenye vitu mbalimbali kwenye jamii yako,  kwa ajili ya kujiletea maendeleo."

Na je kuna uhusiano gani kati ya maendeleo na afya njema ya uzazi?

Judithi anaendelea akisema kuwa, "kwa mfano mkoani Simiyu , kule  unakuta binti anaozwa akiwa na umri wa miaka 9 na binti anakatizwa masomo yake kwa sababu mzazi anataka kupokea mahari ili labda ile mahari imwezeshe kijana wake mwingine kuoa. Kwa hivyo mimi nadhani mila na desturi imekuwa ni changamoto kubwa sana ambayo inarudisha nyuma hivi vitu. Lakini vile vile hawana elimu ya kutosha kwa hivyo unakuta unatumia nguvu sana kuhakikishia anatoka pale  kwenye ile hali aliyonayo kuja katika ile hali ya uelewa."

Audio Credit
Flora Nducha/Devotha Songorwa
Audio Duration
7'15"
Photo Credit
Warren Bright/UNFPA Tanzania