Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini yatimiza miaka 9 ya uhuru inachokijua ni vita badala ya amani:UNHCR

Sudan Kusini yatimiza miaka 9 ya uhuru inachokijua ni vita badala ya amani:UNHCR

Pakua

Leo ni miaka tisa kamili tangu Sudan Kusini taifa changa kabisa duniani lijinyakulie uhuru baada ya kujitenga na Sudan. Lakini tangu lipate uhuru taifa hilo lilichokishuhudia ni vita zaidi ya amani, wimbi kubwa la wakimbizi na sasa linapambana na janga la corona au COVID-19 kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Katika mji wa Ajuong Thok Sudan Kusini wafanyakazi wa shirika la wakimbizi UNHCR wakishirikiana na serikali na wadau wengine wa misaada wanakimbizana na muda kuweza kudhibiti kusambaa kwa janga la COVID-19.

Taifa hili changa kabisa leo Julai 9 linasherehekea uhuru wake huku likiendelea taratibu kujikwamua kutoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenye baada ya kuanzishwa kwa serikali ya mesto mwezi Januari mwaka huu wa 2020, lakini katika baadhi ya maeneo kwa mujibu wa UNHCR vita bado vinaendelea na kutishia juhudi kubwa zilizopigwa kuelekea amani ya kudumu.

Licha ya kutiwa saini kwa mkataba wa amani mwaka 2018 na kuanzishwa kwa serikali ya mesto juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha kila kona ya nchi kuna amani limesema shirika la UNHCR na kuongeza kuwa sasa janga la corona limekuwa tishio jipya hasa ukizingatia kwamba kuna wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 1.7 ambao wanahitaji ulinzi sio tu dhidi ya machafukobali pia dhidi ya COVID-19.

UNHCR na wadau wengine wa misaada ya binadamu wanafanya kila wawezalo kuwalinda wakimbizi hao wa ndani dhidi ya corona na wale walio nje ya nchi zaidi ya 300,000 .

Ingawa kuna matumaini, shirika hilo limetoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini kuongeza kasi ya kusaka amani ya kudumu na kumaliza mgogoro mkubwa zaidi duniani wa wakimbizi wa ndani na wtu waliotawanywa.

Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake kutoka Sudan tarehe 9 Julai 2011 kufuatia kura ya maoni ambapo asilimia 80 ya watu walipiga kura ya ndio ili kujitenga.

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
1'59"
Photo Credit
UNMISS(Picha ya Maktaba July 2018)