Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yayumbisha jahazi la vita dhidi ya ukimwi duniani: UNAIDS Ripoti

COVID-19 yayumbisha jahazi la vita dhidi ya ukimwi duniani: UNAIDS Ripoti

Pakua

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya HIV na ukimwi, UNADS imesema vita vya dunia vya kuhakikisha janga hilo lililokatili maisha ya mamilioni ya watu duniani linatokomezwa, ifikapo mwaka 2030 sasa vinakwenda mrama. Jason Nyakundi na taarifa zaidi

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo ya kuhusu ya hali ya ukimwi duniani, juhudi zinazokwenda kombo ni za kufikia lengo kuu la kutokomeza vitu vitatu katika vita dhidi ya ukimwi ambavyo ni “maambukizi mapya, vifo vinavyohusiana na ukimwi na ubaguzi ifikpo mwaka 2030.”

Akizungumzia kilichochangia hali hiyo mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima amesema “Janga la virui vya corona au COVID-19 limeathiri maisha ya watu na uwezo wao wa kumudu kuishi kila mahali, na wakati gonjwa hilo likisambaa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara  ambako kuna kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU, kuna Ushahidi kwamba watu wanaoishi wa VVU wako katika hatari kubwa ya kupata COVID-19, magonjwa yanayohusiana na janga hilo na hata kufa.”

Ameongeza kuwa hatua za kupambana na janga hilo kama kufunga kila kitu na watu kusalia majumbani pia zimesababisha wagonjwa kufika kliniki na kupata matibabu ya VVU kuwa shida katika nchi nyingi na kubwa zaidi ni pengo la usawa ambalo linahitaji kuzibwa
“Kama tulivyoshuhudia kwa HIV na tunavyoona sasa kwa COVID-19 majanga yanamuathiri kila mtu, lakini hayamuathiriki kila mtu sawa. Ili kupambana na COVID-19, lazima tupambane na pengo la uswa, kwa sababu milipuko ya majanga inapanua zaidi pengo la usawa”

Ripoti hiyo inasema hatari ya VVU miongoni mwa watu wazima iko juu na inatofautiana kwa minajili ya umri, jinsia na kikanda. Kwa mfano Afrika Kusini mwa jangwa la sahara ripoti inasema “wasichana vigori na wanawake wa kati ya umri wa miaka 15-24 ndio walio katika hatari zaidi ya maambukizi mapya ambapo ni mtu 1 kati ya 4."

Kwa kikanda bado Afrika Kusini mwa Jangwa la sahara kunashikilia nafasi ya juu  huku ripoti ikitaja maeneo yalitoathirika zaidi kuwa ni Mashariki na Kusini mwa bara hilo ambako vigori na wasicha ni asilimia 30 ya maambukizi yote mpaya ya HIV duniani. Emile Musabyimana ni mkuu wa kituo cha afya cha Remera mjini Kigali Rwanda ambapo vijana wengi wanakwenda kupima VVU anasema

“Endapo vipimo vya HIV vinarudi kwamba mtu ameambukizwa basi tunawapeleka kwenye ushauri nasaha na kama mgonjwa yuko tayari na anaelewa matibabu ya ARV’s basi wanahamishiwa mara moja kwenye ofisi yetu ya kugawa ARV’s.”

Nje ya Afrika kwa mujibu wa ripoti mwaka 2019 maambukizi mengi mapya yalikuwa miongoni mwa wanaumme karibu robo, au asilimia 23 ya maambukizi mapya yalikuwa ni miongoni mwa wanaumme mashoga Asia na Pasifiki, Amerika ya Kusini, Ulaya Mashariki na Kati na Amerika Kaskazini.

Ripoti pia imetaja kwamba maambukizi yatokanayo na kujidunga madawa ya kulevya kote duniani yalikuwa karibu asilimia 10 ya maambukizi yote mapya. 

Mbali ya changamoto ripoti  imekuwa na Habari njema pia kwamba ongezeko la dawa za kupunguza makali ya VVU limesaidia kuokoa vifo milioni 12.1 vinavyohusiana na ukimwi tangu mwaka 2010.

“Na vifo 690,000 vilisababishwa na ukimwi mwaka 2019 duniani kote  na hiyo ilikuwa ni idadi ndogo zaidi ya vifo vya ukimwi kurekodiwa tangu mwaka 1993 na ni punguzo la asilimia 39 la vifo tangu mwaka 2010." kwa mujibu wa ripoti.

Kwa ujumla ripoti hiyo inasema watu milioni 75.7 wameambukizwa VVU tangu kuanza kwa ugonjwa huo katika miaka ya 1980 na watu milioni 32.7 wamepoteza maisha duniani kote.

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
3'43"
Photo Credit
© UNICEF/Karin Schermbrucke