Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

India, mradi wa IFAD wawanawirisha wanawake wa vijijini

India, mradi wa IFAD wawanawirisha wanawake wa vijijini

Pakua

Kutana na wanawake wa Tejaswini nchini India,  ikimaanisha kwamba ni wanawake walionawiri na kuwezeshwa. Kupitia mradi wa kuwapa mafunzo wa mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD wameweza kujitegemea, kusaidia familia zao , kusaidia na kushamiri. Taarifa inasomwa na Jason Nyakundi.

Katika jimbo la Marastra nchini India wanawake hawa walionawiri au Tejaswini ni sehemu ya wanawake milioni moja wa India walio katika program ya uwezeshaji wanawake vijijini inayofadhiliwa na IFAD.

Kupitia vikundi vya kina mama wanapatiwa mafunzo mbalimbali ikwemo kuanzisha biashara, ufundi na masuala ya uchangishaji fedha. Manjula Gurunath ni mfugaji anakumbuka hali ilivyokuwa kabla ya kujiunga na Tejaswini

“Hapo kabla wanawake walioolewa tulikuwa ni watu wa kuishia katika kuta nne za nyumba zetu, na baada ya kujiunga na kikundi cha kusaidiana ndipo nikababaini kwamba kuna maisha zaidi ya hizo kuta nne na kwamba sikustahili kuendelea kubakia kizani.”

Kwa wanawake kama Manjula maisha nje ya kuta za nyumba zao yamewapa mafanikio ya kifedha , kujiamini na kuweza kujitegemea. 

Kupitia ufadhili wa IFAD vikundi vidogovidogo wa kusaidiana vilianzishwa na mbali ya kupewa mafunzo wanachama wanaweza pia kupatiwa mikopo kama aliopewa Kanta Ashok Thorwe ambaye pia alipata mafunzo ya kutengeneza sahani anasema“Tulichukuwa mikopo kwenye vikundi vya kusaidiana tukanunua mashine ya kutengeneza sahani za karatasi na baada ya kununua mashine hiyo tuliweza kutengeneza sahani nyingi zaidi kwa siku. Tulipiga mahesabu ya gharama zetu na faida yetu ilikwenda juu.”

Karibu kila kikundi kiliweza kupata mkopo na kuwawezesha wanachana kufadhili biashara zao.  Sasa wamefanikiwa sana na kufikia hatua ya kukopeshana faida wanayoipata.

Na ujuzi wanaoupata hawaukalii wanausambaza kwa wanawake wenzao, kama anavyofanya Sangeeta S. Chowghe fundi cherahani “Tangu biashara yangu ya cherahani ilipokuwa nimeanza kufundisha wanawake wengine. Nilianza kupata fedha zaidi na hii imenisaidia kuwapa watoto wangu elimu bora”

Kupitia vikundi hivyo wanawake pia wanajadili changamoto zinazowakabili na kuzipatia suluhu kama jamii.

Hivi sasa mafanikio yao sio tu kwenye biashara tu, wanawake hawa wa Tejaswini wanachukua majukumu mbalimbali ya kijamii na kisiasa na wamekuwa na mnepo mkubwa hasa wakati huu wa janga la corona au COVID-19 kwa kubadili mwenendo wa biashara zao kukabiliana na hali halisi.

 

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'38"
Photo Credit
UN Development Programme