Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi, kampeni ya UNICEF yaweka wazi baba wa kipekee

Malawi, kampeni ya UNICEF yaweka wazi baba wa kipekee

Pakua

Nchini Malawi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linapigia chepuo kitendo cha mzazi wa kiume kusaidiana na mzazi mwenzake katika malezi na makuzi ya watoto wao ili hatimaye watoto hao waweze kukua si tu kimwili bali pia kifikra.

Miongoni mwa familia hiyo ni ile ya Shemison Banda, mkazi wa mji mkuu wa Malawi, Lilongwe, ambaye kupitia kampeni ya UNICEF ya Baba wa Kipekee anasema kuwa yeye na mke wake wana watoto wawili wa kike na alianza kuwahudumia tangu wakati wa ujauzito wa mama yao.

Thereza Banda, mwenye umri wa miaka 9, ni mtoto wa pili wa Bwana Banda na anasema kuwa, “baba yangu ni baba wa kipekee kwa sababu nikimwambia tucheze mpira, tunacheza na pia kuna wakati ananisaidia kazi zangu za shuleni. Na ni kwa sababu hiyo, watoto wenzangu wananiambia kuwa baba yako ni baba wa kipekee. Na mimi nawaambia kuwa baba yangu ni baba wa kipekee kwa sababu ananipenda sana, na mimi ninampenda sana.”

Mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto unataja misingi mikuu minne ya haki za mtoto ambayo ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa ambapo Bwana Banda anasema kuwa, “nilianza kuwalea hata kabla hawajazaliwa. Nilimtunza mama yao wakati mjamzito. Na hata baada ya kuzaliwa niliendelea kuwatunza. Miongoni mwa mambo ninayokumbuka kuwafanyia ni kuwaogesha, kuwabadilisha nguo walipojisaidia, kuwabembeleza walipolia, kuwalaza kitandani, kuwabeba mgongoni na kubakia nao nyumbani pindi mama yao alipokwenda kazini.”

Kaul iza Bwana Banda zinathibitishwa na mkewe aitwaye Judith Banda ambaye anasema kuwa, “mume wangu ananisaidia watoto na pia kuhudumia nyumba yetu. Nikipika, yeye anasafisha nyumba.”

Kwa binti yao wa mkubwa, Amazing mwenye umri wa miaka 14, baba yake na mama yake wote ni wazazi wa kipekee ana anasema kuwa “nikiwa mkubwa nataka niwe kama mama, mama yangu ni muuguzi, na baba yangu ni wa kipekee kwa sababu kwa tabia zake nafiriki ni baba wa kipekee.”

Bwana Banda anasema kuwa yeye anacheza na watoto wake kwa sababu inasaidia kukuza na kuendeleza ubongo wao na kwamba, “kwa wao kukua, lazima niwafundishe kupitia vile vitu ambavyo ninavifanya. Na hii itawasaidia kwa changamoto za usoni. “
 

 

Audio Credit
Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
1'58"
Photo Credit
UNICEF/Sebastian Rich