Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yafikisha msaada wa COVID-19 kwa nchi zaidi ya 100 licha ya changamoto

UNICEF yafikisha msaada wa COVID-19 kwa nchi zaidi ya 100 licha ya changamoto

Pakua

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema licha ya changamoto lukuki limefanikiwa kufikisha msaada kwa nchi zaidi ya 100 kupambana na janga la corona au COVID-19 na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu. 

Katika ripoti yake iliyotolewa leo mjini New York na Copenhagen, UNICEF imesema wakati janga la COVID-19 likipindua maisha ya mamilioni ya watoto kote duniani , UNICEF inafikisha msaada wa kuokoa maisha licha ya kukabiliwa na vikwazo vingi na vikubwa ikiwemo masuala ya usafiri na matatizo ya kiufundi.

Henrietta Fore mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo amesema “Kuanzia uhaba wa bidhaa hadi changamoto za usafiri, COVID-19 imeleta mtihani mkubwa katika operesheni zetu. Hata hivyo kwa msaada kutoka kwa washirika wetu tumeweza kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu na kuwalinda watoto na jamii zao.”

Hadi kufikia sasa mwaka huu UNICEF imeshasafirisha vifaa vya msaada wa kujikinga na corona (PPE) kwa zaidi ya nchi 100 kwa lengo la kusaidia mapambano dhidi ya janga hilo ikiwemo barakoa milioni 7.5, mashine za Oksijeni zakusaidia kupumua milioni 2.8, karibu glavu milioni 10, magauni ya hospitali 830,000 na karibu vifa vingine laki sita vya kujikinga kwa wahudumu wa afya.

UNICEF pia imesafirisha makasha zaidi ya laki tano na nusu ya kupima corona na mengine zaidi ya laki tisa yanatarajiwa kusambazwa ifikapo mwezi Agosti.

Na shirika hilo lintarajia kupeleka mashine zingine za oksijeni zaidi ya 16,000 ktika nchi 90 za kipato cha chini na cha wastani.

Vikwazo vya usafiri kutokana na hatua za kupambana na COVID-19 shirika hilo linasema vimetia dosari kubwa katika operesheni zao likitoa mfano wa usafirishaji wa chanjo kati ya Machi na Mei kila mwaka hufanikiwa kufanya safari zaidi ya 700 za kusafirisha chanjo kwenye nchi mbalimbali lakini kipindi hichohicho mwaka huu 2020 ni safari 391 pekee ndio zilizoweza kufanyika.

Ili kushughulikia changamoto hiyo ya kusafirisha chanjo UNICEF inatoa wito kwa serikali, sekta binafsi, sekta ya usafiri wa anga na wengineo kutoa suluhu ya usafiri wa anga kwa ajili ya kuhakikisha chanjo hizo za kuokoa maisha zinawafikia mamilioni ya watu na hasa watoto wanaozihitaji zaidi.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'10"
Photo Credit
© UNICEF