Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila mabaharia uchumi wa dunia hauwezi kufanya kazi-Guterres

Bila mabaharia uchumi wa dunia hauwezi kufanya kazi-Guterres

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya mabaharia duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuwapa mabaharia heshima wanayoistahili.

Bwana Guterres  kupitia ujumbe wake kuhusu siku hii ya mahabaria amesema mabaharia ni moja ya mashujaa wa dunia ambao hawazungumziwi na hivyo akatoa wito kwa jamii kuwa sasa ni wakati muafaka kuwapa heshima wanayoistahili kwani walionesha umuhimu mkubwa kwa kuendelea kutoa huduma muhimu ya usafirishaji wakati wa janga la ugonjwa wa COVID-19.

“Mabahari  wameendelea kutoa huduma hii muhimu katika hali ngumu isiyo ya kawaida iliyoletwa na janga la COVID-19. Hata katika nyakati nzuri zaidi, mabaharia hufanya kazi muda mrefu mbali na nyumbani, kwa kiasi kikubwa mchango wao  haujatambuliwa.” Amenukuliwa Guterres kuhusu siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 mwezi Juni.

Bwana Guterres ameeleza kuwa mwaka huu, zaidi kuliko wakati mwingine wowote, nchi zote duniani zinatakiwa kuwaenzi mabaharia kwa kuwatambua kama wafanyakazi muhimu na kuwapatia usaidizi wa kusafiri ili kuhakikisha usalama. Aidha Guterres ameleeza kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kazi ILO yameweka itifaki ya kutekeleza hatua hizo na hivyo akazisihi serikali duniani kutekeleza.

Naye Katibu Mkuu wa shirika la kimataifa la shughuli za usafirishaji wa majini IMO Kitack Lim katika ujumbe wake kuhusu siku hii alioutoa kwa njia ya video amesema kuwa kama walivyo wafanyakazi wengine muhimu, wako mstari wa mbele katika kupambana na janga la COVID-19 na wanastahili asante na usaidizi wa kibinadamu kutoka serikali zote duniani siyo tu wakati huu wa janga, bali wakati wote.

Bwana Lim ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 mabaharia wamekumbana na changamoto nyingi ikiwemo kukosa huduma za kiafya na hata kukosa kuruhusiwa kutoka katika meli zao kwenda nchi kavu lakini wameendelea kuuhudumia ulimwengu,

“Pamoja na changamoto zote hizo, mabaharia wamebaki kazini saa 24, siku 7 za wiki. IMO imeshirikiana na nchi wanachama, vyama vya wafanyakazi, mashirika ya mabaharia, tasnia ya usafirishaji majini na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kutafuta suluhisho la matatizo haya. Nimekuwa nikiwasihi wanachama wote wa IMO kuwatambua mabaharia kama wafanyakazi muhimu.”

Akisisitiza kuhusu umuhimu wa shughuli ya ubaharia, Bwana Lim amesema zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya dunia inafanyika kupitia katika bahari na ni mabaharia wanaofanikisha hilo kupitia kazi yao ngumu inayomuhitaji mtu kimwili na kiakili.

Audio Duration
2'46"
Photo Credit
Picha/ IMO