Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA yabisha hodi magerezani CAR

MINUSCA yabisha hodi magerezani CAR

Pakua

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP wamepatia gereza la Ngaragba msaada wa vifaa vya kusaidia kuepusha kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 gerezani humo. Loise Wairimu na maelezo zaidi.

Kauli ya mgeni njoo mwenyeji apone, imekuwa bayana katika gereza la Ngaragba, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, kwa kuwa ujio wa maafisa wa MINUSCA na UNDP ni ahueni kwa wafungwa na wafanyakazi wa gereza hili katika kujikinga na COVID-19.

Gharama ya msaada huu unaolenga wafanyakazi na wafungwa ni dola 120,000  na unajumuisha glovu, dawa za kupuliza, barakoa, vipima joto vinavyotumia mionzi, sabuni, dawa za kutakasisha mikono na magauni ya kujikinga.

Joël Hubert Yandome, ni msimamizi wa gereza hili la Ngaragba.

Tunafurahia sana kupokea msaada huu. Huu ugonjwa hauna mipaka. Wafungwa na wafanyakazi wa gereza wanaweza kuambukizwa. Wafungwa wanaweza kufa kwa COVID-19. Tunafurahia sana kitendo hiki cha kikarimu kutoka kwa wadau wetu.”

Kwa kutumia vifaa hivyo, wafungwa na wafanyakazi wanaweza kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao hadi sasa katika taifa hilo la Jamhuri ya Afrika ya Kati kuna wagonjwa 2,410 waliothibitishwa na kati yao hao 14 wamefariki dunia.

Je msaada huu unakomea kwa gereza hili pekee? Leila Ben Othman ni mkuu wa kitengo cha masuala ya magereza, MINUSCA.

 “Hii ni awamu ya kwanza, magereza yote 12 nchini CAR yatapatiwa msaada wa aina mbalimbali ya vifaa vya kinga na vya kujisafi.”

MINUSCA pamoja na kusaidia kuimarisha ulinzi wa raia, inasaidia pia masuala ya mchakato wa uchaguzi na masuala ya kibinadamu na kijamii.

Audio Credit
Flora Nducha/Loise Wairimu
Audio Duration
1'53"
Photo Credit
MINUSCA