Kikosi cha Tanzania nchini DRC,TANZBATT 7 chatoa msaada hospitali kuu Beni

15 Juni 2020

Hospitali kuu ya Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imeshukuru msaada wa dawa kutoka kikosi cha Tanzania kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini  humo, MONUSCO  ikisema kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka. Ripoti zaidi na Issa Mwakalambo, afisa habari wa kikosi hicho cha Tanzania huko Beni.

Katika hospitali hii ya dayosisi ya Butembo mjini Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walinda amani kutoka kikosi cha 7 cha Tanzania, TANZBATT 7,  kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, wamefika kwa ajili ya kuwasilisha msaada wa dawa.

Dkt. Frank Muhindo Fikiri ni Mkurugenzi wa hospitali hii anasema, "eneo hili linadhulumiwa sana  kwa vita,kwa mashambulizi,  wakimbizi watoto wachanga wanaokosa malisho, wazazi akina mama wanaojifungua bila msaada wowote.Tunafurahi na tunaona hiyo msaada mdogo utasaidia kuongeza uwezo wetu wa kuwahudumia wangonjwa mbalimbali wanaopatikana hapa hospitali."

Kwa upande wake, Dkt Joseph Mkandara kutoka TANZBATT 7, anafafanua kuhusu msaada wao, "kwa dawa kiasi kwa ajili ya kuwasidai wangonjwa waliopo hapa hospitali ya Beni ,ni dawa kidogo lakini tunaimani kwamba zitawasaidia."

Private Jenifa Mbogo ni mlinda amani kutoka Tanzania anasema,  "tumekuja hapa hospitali ya Beni ili kuleta dawa kama msaada ili kuwasaidia akina mama pamoja na watoto."

Audio Credit:
Issa Mwakalambo
Audio Duration:
2'33"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud