ILO na UNICEF zasema COVID-19 huenda ikawatumbukiza mamilioni zaidi katika ajira ya Watoto

12 Juni 2020

Ikiwa leo ni siku ya kupinga ajira ya watoto duniani, taarifa ya pamoja iliyotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa imesema janga la virusi vya corona au COVID-19 linatishia mafanikio yaliyopatikana kote duniani ya kupunguza ajira ya watoto kwa idadi ya milioni 94 tangu mwaka 2000.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa imesema janga la virusi vya corona au COVID-19 linatishia mafanikio yaliyopatikana kote duniani ya kupunguza ajira ya Watoto kwa milioni 94 tangu mwaka 2000.

Mashirika hayo la kuhudumia Watoto UNICEF na la kazi duniani ILO kwenye taarifa yao ya Pamoja yamesema hivi sasa duniani kote wasichana na wavulana milioni 151 wa umri wa kati ya miaka 5-17 wako katika ajira ya Watoto na asilimia 70 kati yao wanafanyakazi katika sekta ya kilimo ikiwemo ukulima, ufugaji, masuala ya misitu, uvuvi na ufugaji samaki.

Hatari inayochangiwa na COVID-19

Kwa mujibu wa taarifa ya mashirika hayo ilitolewa mahusus kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kupinga ajira ya Watoto duniani ambayo kila mwaka huwa Juni 12, mamilioni zaidi ya watoto wako katika hatari ya kutumbukia kwenye ajira ya watoto kwa sababu ya janga la COVID-19 ambalo linaweza kusababisha ongezeko la kwanza la ajira ya Watoto baada ya miaka 20 ya hatua kubwa za kupunguza tatizo hilo.

Ripoti ya utafiti ya mashirika hayo mawili iitwayo “COVID-19 na ajira ya Watoto wakati wa mgogoro , wakati wa kuchukua hatua” ajira kwa kwatoto ilipungua kwa kiasi kikubwa lakini sasa mafanikio hayo yako hatarini.

Imeongeza kuwa Watoto ambao tayari wako katika ajira huenda wanafanyishwa kazi kwa masaa mengi au katika mazingira magumu.

Wengi wao huenda wanashinikizwa kuingia katika mifumo mibaya zaidi ya ajira ambayo husababisha madhara kwa afya na usalama wa watoto hao.

UNICEF/Prashanth Vishwanathan
Mvulana ambaye alilazimika kufanya kazi katika kiwanda huko Hyderabad, India anapigwa picha nje ya nyumba yao.

Changamoto ya COVID-19 kwa ajira ya Watoto

Akizungumzia changamoto ya COVID-19 kwa ajira ya Watoto mkurugenzi mkuu wa ILO amesema “Wakati janga la COVID-19 likisababisha zahma katika kipato cha familia bila msaada wengi watageukia ajira ya Watoto.Hivyo hifadhi ya kijamii ni muhimu sana wakati wa majanga kwani inatoa msaada kwa wale ambao wako hatarini zaidi. Kwa mantiki hiyo kujumuisha hofu za ajira ya Watoto katika sera zote kwa ajili ya elimu, hifadhi ya jamii, haki, soko la ajira na haki za kimataifa za binadamu za ajira italeta tofauti kubwa.”

Kwa mujibu wa ripoti yao janga la COVID-19 linaweza kusababisha ongezeko la umasikini na hivyo ongezeko la ajira ya watoto wakati familia nyingi zikitumia kila njia kuweza kuishi.

Utafiti mwingine umeonyesha kwamba ongezeko la umasikini kwa asilimia 0.1 unasababisha ongezeko la ajira kwa Watoto kwa asilimia 0.7 katika baadhi ya nchi.

Naye mkuu wa UNICEF Henrietta Fore kwa upande wake amesema “Wakati wa majanga ajira kwa Watoto ndio inaonekena njia ya kujikomboa kwa familia nyingi. Wakati umasikini unaongezeka , shule zimefungwa na upatikanaji wa huduma za kijamii ukipungua Watoto wengi wanalazimika kuingia katika soko la ajira. Wakati tunaibuka kutoka kwenye janga la COVID-19 tunahitaji kuhakikisha kwamba watoto na familia zaowana nyenzo wanazohitaji kuhimili janga kama hili katika siku za usoni. Elimu bora, huduma za hifadhi ya jamii na fursa za uchumi bora vitabdili kabisa mwelekeo.”

 

Audio Duration:
2'54"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud