Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka koroboi hadi taa za sola Ziwa Victoria

Kutoka koroboi hadi taa za sola Ziwa Victoria

Pakua

Nchini Tanzania shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP limesaidia juhudi za kusambaza nishati jadidifu kwa wavuvi ili kupunguza uchafuzi wa mazingira utokanao na uvuvi wa kutumia koroboi za mafuta ya taa katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza.

Mkurugenzi wa kampuni ya Millennium Engineers Diana Mbogo, ambao ni wanufaika wa mradi wa UNEP amemweleza Ahimidiwe Olotu wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa jijini Dar es salaam manufaa ya taa hizo za sola,

“Ziwa Victoria hutoa hewa ya ukaa kiasi kikubwa kuliko hata taifa la Burundi kutokana na uvuvi unaotumia koroboi na mafuta ya taa. Sasa kutumia sola kunamaanisha kuwa, hewa ya ukaa haichafui tena mazingira. Tunaepusha tani nyingi za hewa ya ukaa isirudishwe tena kwenye mazingira kutokana na kutotumia yale mafuta ya taa. Kwa hiyo wakati anatumia teknolojia hii anakuwa anaokoa mazingira wakati huo.”

Hivi sasa wanashirikiana na serikali kuanzia za mitaa hadi za mkoa ili kuelimisha jamii za wavuvi hususan zile zilizo pembezoni zaidi kuhusu umuhimu wa teknolojia hiyo. Na je mgao wa taa hizo uko vipi?

“Sasa hivi tulikuwa tunawafikishia kwa pamoja na mwaka huu ni awamu ya majaribio ili kuona je wataipokeaje hii teknolojia napia wataitumiaje na pia njia mbalimbali ambazo wanaweza kutumia kwa njia rafiki Ili tuweze kukaribisha sekta binafsi na serikali ili waweze kufanya kazi kwa pamoja kupitia mianya sahihi ya kibiashara.”

Lengo namba 7 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, linataka kuwepo kwa teknolojia nafuu za nishati kama vile jadidifu ili wananchi waweze kumudu na hatimaye wachangie katika kupunguza utoaji hewa chafuzi kama ya ukaa na hatimaye kulinda tabianchi.

Audio Duration
2'10"
Photo Credit
UN Tanzania