Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 inatupa fursa na wajibu wa kuimarisha uhusiano wetu na asili: Guterres

COVID-19 inatupa fursa na wajibu wa kuimarisha uhusiano wetu na asili: Guterres

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya bahari duniani , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema janga la virusi vya Corona au COVID-19 ni kumbusho kwamba binadamu wote wanahusiana wenyewe lakini pia na asili. Tupate ufafanuzi zaidi na Jason Nyakundi

Guterres ameyasema hayo kupitia ujumbe wake maalum wa siku hii ambayo kila mwaka huadhimishwa June 8 na kusistiza kwamba wakati dunia ikijitahidi kukomesha janga hili la COVID-19 na kujijenga upya ni fursa muhimu ya kubadilika

“Tuna fursa ya kipekee katika kizazi hiki na wajibu wa kurekebisha uhusiano wetu na ulimwengu wa asili ikiwemo bahari za dunia hii. Tunazitegemea bahari kwa chakula, maisha, usafiri na biashara”

Katibu mkuu ameongeza kuwa wakati mapafu ya dunia hii na kiwango chake kikubwa cha hewa ukaa vikididimia, bahari ina jukumu muhimu sana katika kukabili mabadiliko ya tabianchi lakini

“Leo hii kina cha bahari kinaongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kutishia uhai na maisha katika mataifa madogo na miji ya mwambao na jamii kote duniani. Tindikali inaongezeka baharini na kuweka bayoanuwai ya bahari na mnyororo muhimu wa chakula hatarini.”

Kana kwamba hayo hayatoshi Guterres amesema, uchfuzi utokakanao na taka za plastiki umetapakaa kila mahali.

Mwaka huu siku ya bahari imejikita katika ubunifu kwa ajili ya maendeleo endelevu, na Katibu Mkuu anasisitiza kwamba uelewa mzuri wa bahari ni muhimu kwa ajili ya kuhifadhi akiba ya samaki na kubaini bidhaa mpya na madawa.

 Kwa mantiki hiyo amesema muongo wa Umoja wa Mataifa wa sayansi ya bahari kwa ajili ya maendeleo endelevu unaokuja hivi karibuni utatoa taswira ya mkakati wa pamoja wa kuchukua hatua kwa ajili ya bahari.

 Hivyo amezitaka serikali na wadau wote kuahidi na kujikita na uhifadhi na uendelevu wa bahari kupitia ubunifu na sayansi.

Audio Duration
1'56"
Photo Credit
UNDP/Azza Aishath