Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tubadili tabia tulinde mazingira kwa kuwa muda unayoyoma - Guterres

Tubadili tabia tulinde mazingira kwa kuwa muda unayoyoma - Guterres

Pakua

Mazingira yanatutumia ujumbe dhahiri ya kwamba tunaharibu mazingira yetu ya asili kwa hasa yetu wenyewe,  hivyo ndiyo alivyoanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya mazingira duniani hii leo Juni 5, maudhui yakiwa bayonuai. John Kibego na ripoti kamili.

Mwaka huu maadhimisho ya siku ya mazingira duniani, yanafanyika kukiwa na matukio ya kutia hofu kama vile mioto ya nyika nchini Brazil, Marekani na Australia na baa la nzige Mashariki mwa Afrika na sasa janga la COVID-19, hali ambayo Umoja wa Mataifa inasema kuwa inaonesha uhusiano mkubwa kati ya binadamu na mazingira.

Ndio maana Katibu Mkuu Guterres katika ujumbe wake anasema kuwa uharibifu wa mazingira na bayonuai vinafanyika kwa kasi kubwa huku tabianchi nayo inazidi kusambaratika kila uchao.

"Mioto, mafuriko, ukame na vimbunga vikubwa kupita kiasi vinatokea mara kwa mara hivi sasa na vinasababisha uharibifu. Kiwango cha joto na aside baharini kinaongezeka huku vikiharibu mifumo anuai ya matumbawe. Na sasa virusi vipya vya Corona vinaharibu afya na mbinu za kipato.”

Guterres anasema kuwa, kutunza ubinadamu ni lazima kutunza mazingira na kwamba jamii nzima ya kimataifa inatakiwa kubadili mweleko akisema,

 Hebu tufikirie upya kile tununuacho na  tutumiavyo. Tufuate mbinu endelevu , kwenye kilimo na kwenye biashara Tulinde maeneo yaliyosalia ya wanyapori na tuahidi mustakabali usioharibu mazingira na wenye mnepo.”

 Bwana Guterres anasema kuwa wakati huu jamii ya kimataifa inafanya kazi kurejesha hali bora,

“Hebu na turejeshe mazingira katika hali yake, yawe kitovu cha hatua zetu za kupitisha maamuzi. Na katika siku ya mazingira duniani hii leo ni wakati wa mazingira.”

 Siku ya mazingira duniani ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 15  mwezi Desemba mwaka 1972 kupitia azimio namba A/2994.

 

Audio Duration
2'3"
Photo Credit
Unsplash/Habib Dadkhah