Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko, nzige na COVID-19 vyatishia kuirudisha nyuma Somalia:OCHA

Mafuriko, nzige na COVID-19 vyatishia kuirudisha nyuma Somalia:OCHA

Pakua
Mafuriko, nzige na COVID-19 vyatiashia kuirudisha nyuma Somalia:OCHA 

 Somalia taifa lililoghubikwa na miongo zaidi ya mitatu ya vita vinavyoendelea sasa mafuriko, nzige na janga la corona au COVID-19 vinatishia kurudisha nyuma hatua kubwa zilizopigwa za kisiasa na kiusalama, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misada ya dharura OCHA. Tupate maelezo zaidi na Jason Nyakundi

Katika mitaa ya mji wa Belet weyne jimbo la Katikati mwa Somalia mafuriko yametapakaa kila kona kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Kwa mujibu wa OCHA takribani watu 500,000 wametawanywa kutokana na mafuriko hayo ambayo yameathri jumla ya watu zaidi ya milioni moja na kusambaratisha biashara , mazao, masoko, na kuwaacha wengi wakipoteza kila kitu , kushindwa kumudu gharama za chakula na kukosa kipato . Miongoni mwao ni Hawa Gedi mama wa watoto wanne ambaye baada ya kupoteza nyumba yake sasa anapata hifadhi katika makazi ya wakimbizi wa ndani ya Ceel Jaaele

“Nilitawanywa na mafuriko huko Bula Qodah na nikapewa malazi hapa Ceel Jaale, tunashukuru sama mashirika ya misaada ya kibinadamu kwa kutupa maji na mahitaji mengine ya msingi, lakini tunahitaji msaada zaidi, tunahitaji chakula, hatuna chochote cha kula.”

Kana kwamba vita na mafuriko havitoshi zahma ya nzige nayo inawazonga, OCHA inasema wakulima wengi Somalia wamepoteza mazao yao yote .

Na sasa janga la COVID-19 limezusha taharuki nyingine mpya huku mkuu wa OCHA Somalia Justin Brady akionya kwamba mfumo wa Somalia ni dhaifu kuweza kukabiliana na majanga yote haya kwa pamoja ukilinganisha na mataifa jirani hali ambayo inatia wasiwasi mkubwa wa kurudisha nyuma hatua zote zilizopigwa kisiasa na kiusalama kwa miongo kadhaa iliyopita na kuiweka tena jamii njiapanda.

“Tunakabiliwa na hali ya matatizo mawili ya mafuriko na COVID-19 ambayo yanazidisha athari kwa watu, na kisha tuna nzige. Tunatarajia kushuhudia sehemu ya mazao mwaka huu yakipotea kutokana na nzige hali ambayo itaathiri uhakika wa chakula na lishe kwa Wasomali wengi.”

Kwa sasa shirika la afya duniani WHO linafanyakazi kwa karibu na OCHA na serikali ya Somalia kudhibiti kusambaa kwa COVID-19 . Jumla ya wagonjwa zaidi ya 2,080 wa corona na vifo karibu 80.

Umoja wa Mataifa na serikali wanahitaji dola milioni 57 kwa ajili ya operesheni za kibinadamu na kukabilana na majanga hayo matatu Somalia, lakini hadi sasa fedha zilizopatikana ni asilimia 20 pekee.

Audio Duration
2'42"
Photo Credit
UN Photos