Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahisani wa kimataifa wakutana kuchangisha fedha kuinusuru Yemen:UN

Wahisani wa kimataifa wakutana kuchangisha fedha kuinusuru Yemen:UN

Pakua

Wahisani wa kimataifa wanakutana leo katika mkutano ulioitishwa na Ufalme wa Saudi ana Umoja wa Mataifa ili kuchangisha fedha kwa ajili hatua za kibinadamu kunusuru Maisha ya mamilioni ya watu nchini Yemen. Jason Nyakundi antupasha zaidi.

Mkutano huo unaofanyika kwa njia ya mtandao umewaleta Pamoja zaidi ya serikali 130 na wahisani wengine, mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu na maafisa wa misaada ili kuweka bayana hali halisi ya kibinadamu  inayozorota kwa kasi ambako mbali ya zahma zingine zinazowakabili janga la virusi vya Corona au COVID-19 ni changamoto mpya inayowasibu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa lengo kubwa la mkutano huo wa uchangishaji fedha ni kutangaza ahadi za kifedha kwa ajili ya kuendelea na operesheni za kibinadamu Yemen.

Mkutano huo umekuja wakati ambapo hali kwa raia wengi wa Yemen ni mbaya sana kuliko ilivyowahi kuwa katika wakati wowote ule kwenye historia ya nchi hiyo.

Mipango mingi ya misada ya kibinadamu sasa iko njiapanda kutokana na ukata wa fedha. Hivi sasa Yemen ndio mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani ikiwa na watu milioni 24 wanaohitaji msaada na ulinzi na hali inazidi kuwa mbaya kila uchao.

Mazingira yaliyopo yanaashirikia janga la COVID-19 kusambaa haraka, nchi zima na kuulemea mfumo wa afya. Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yasiyo ya kiserikali NGOs yanahitaji dola bilioni 2.4 kushughulikia mahitaji ya kibinadamu Yemen hadi mwisho wa mwaka huu ikiwemo dola milioni 180 kwa ajili ya kupambana na COVID-19.

Hali halisi ni kwamba fedha zinapelea kwa kiasi kikubwa na kati ya program 41 za misaada ya kibinadamu Yemen zaidi ya 30 zitafungwa katika wiki chache zijazo endapo fedha zinazohitajika hazitopatikana na hivyo kuwaacha mamilioni ya watu bila msaada wanaouhitaji ili kuishi.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Mark Lowcock amesema “ Hali nchi Yemen ni mbaya sana lakini bado tuna uwezo wa kuwafikia watu. Kuna maelfu ya wafanyakazi wa misaada raia wa Yemen ambao bado wanafanyakazi na Umoja wa Mataifa, Shirika la msalaba mwekundu na NGOs. Lakini mengi ya mashirika hayo yamesalia na muda mfupi tu kabla ya kuishiwa. Tunawaomba wahisani sio tu kutoa ahadi ya fedha leo lakini kulipa ahadi hizo haraka”.

Umoja wa Mataifa umesema umesaliwa na dola milioni 698 tu kwa ajili ya operesheni zote za misaada Yemen, hivyo dola bilioni 2.4 zinazoombwa na Umoja wa Mataifa ni za kuziba pengo lililosalia hadi mwisho wa mwaka huu. Mkutano kama huo mwaka jana ulichangisha dola bilioni 2.6.

Audio Duration
2'13"
Photo Credit
UN OCHA/GILES CLARKE