Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunawapatia wanawake DRC stadi za ujasiriamali– Private Anna

Tunawapatia wanawake DRC stadi za ujasiriamali– Private Anna

Pakua

Mlinda amani mwanamke kutoka Tanzaina ambaye anahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO,  amethibitisha umuhimu wa uwepo wa askari wa kike katika ulinzi wa amani katika taifa hilo lililogubikwa na mizozo. Loise Wairimu na ripoti kamili.

Private Anna Malima Musa wa kikundi cha 7 cha TanzaniaTANZBATT 7,  kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi cha MONUSCO, FIB amesema hayo wakati huu ambapo dunia hii leo inasherehekea siku ya walinda amani ulimwenguni, ujumbe ukiwa wanawake walinda amani ni ufunguo wa amani ya kudumu.

Akizungumza kutoka makao makuu ya kikosi hicho huko Beni, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, Private Anna amesema kuwa

“Wanawake wana changamoto nyingi kama magonjwa na unakuta hawezi kumwelezea mwanaume. Unakuta mama ana magonjwa lakini hajui afanye nini kutokana na mazingira magumu na hana uwezo wa kwenda hospitali. Hivyo tukikutana nao tunawapa elimu ya jinsi ya kujikinga, hususan hili gonjwa la COVID-19, tumewapa elimu ya kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kutumia barakoa.”

Na akaenda mbali zaidi kuhusu msaada wao kwa wanawake wenye watoto lakini hawana njia ya kipato akisema,

“Unakuta ni mama hana mume, ila ana kundi la watoto, hivoy tunawapatia elimu ya kujishughulisha, mfano ushonaji, upandaji wa maua na anaweza kujishughulisha hata ufumaji na hatimaye akapata kipato cha kuweza kupeleka watoto shule.”

 TANZBATT 7,  ina jumla ya wanajeshi 949 na miongoni mwao 63 ni askari wa kike.

Kikosi hicho cha Tanzania kinahudumu kwa mwaka mmoja na kinatarajia kukamilisha kazi yake mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020.

Umoja wa Mataifa umeangazia walinda amani wanawake mwaka huu ikiwa ni miaka 20 tangu kupitishwa kwa azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2020 likitaka mchakato wowote wa amani na usalama ikiwemo operesheni za ulinzi wa amani zijumuishe walinda amani wanawake.

 

 

Audio Duration
2'56"
Photo Credit
TANZABATT 7/Ibrahim Mayambua