Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde tushikamane kuchangia na kuwanusuru Wasyria na COVID-19:IOM

Chonde chonde tushikamane kuchangia na kuwanusuru Wasyria na COVID-19:IOM

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema fedha za ufadhili kwa ajili ya maelfu ya raia wa Syria waliotawanywa na machafuko inasalia kuwa kipaumbele kinachotia hofu kubwa ya utoaji msaada wa kibinadamu hasa wakati huu ambapo janga la virusi vya corona au COVID-19 linaongeza msumari wa moto juu ya kidonda. Loise Wairimu na taarifa kamili

Kwa mujibu wa shirika hilo la IOM, watu wa Syria wameingia mwaka wa 10 wa vita mwezi Machi mwaka huu na sasa wanalazimika kukabiliana na janga lingine linalotoa tishio kubwa ambalo ni mlipuko wa COVID-19. Janga hili linatishia maisha ya watu milioni 11 ambao tayari kwa sababu ya vita wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Akizungumzia umuhimu wa msaada kwa watu hao wa Syria mkurugenzi mkuu wa IOM António Vitorino.    Amesema “Ni lazima tujiandae kukabiliana na tishio la COVIDI-19 kwa jamii ambazo tayari zinahaha kujikwamua na vita na mamilioni ya watu kutawanywa. IOM hivi sasa inapanua wigo wa hatua zake za msaada kwa jamii zilizo katika hali mbaya huku ikichukua hatua za kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya COVID-19, kupunguza athari za kiuchumi kwa maisha ya watu na kuzisaidia jamii kujiandaa na miapango ya muda mrefu ya kujikwamua.”

Serikali ya Syria imeripoti wagonjwa 121 hadi sasa waliothibitishwa kuwa na COVID-19, ingawa hakuna mgonjwa aliyeorodheshwa katika eneo la Kaskazini Magharibi lenye machafuko makubwa, afya na usalama wa watu zaidi ya milioni moja wanaoishi katika mahema yaliyofurika, bila huduma za msingi ndio suala linalotia hofu kubwa.

Hivi sasa IOM inatoa wito wa mshikamano kutoka kwa wahisani kote duniani kusaidia mahitaji ya jumla ya watu milioni 3 ambao ni wakimbizi  na wakimbizi wa ndani Syria kupitia ombi la dola milioni 206.

Kati ya fedha hizo IOM inasema dola milioni 33 zitaelekezwa katika juhudi za kupambana na COVID-19 na athari zake.

Audio Duration
2'1"
Photo Credit
Picha ya UN