Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yawa upenyo wa kutangaza maziwa ya kopo badala ya maziwa ya mama- Ripoti

COVID-19 yawa upenyo wa kutangaza maziwa ya kopo badala ya maziwa ya mama- Ripoti

Pakua

Ripoti mpya ya mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau, inaonesha kuwa juhudi za kukomesha matangazo ya maziwa ya kopo kwa ajili ya watoto wachanga zinaendelea kukumbwa na mkwamo hasa wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19. Jason Nyakundi na ripoti kamili.

 Ripoti hiyo ikiwa imeandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF, la afya WHO na mtandao wa kimataifa wa hatua kuhusu chakula cha mtoto, IBFAN, inasema kuwa maziwa ya mama yanakumbwa na vikwazo kutokana na fikra potofu ya kwamba yanaweza kusababisha maambukizi ya virusi vya Corona kwa mtoto.

 WHO na UNICEF kupitia taarifa iliyotolewa leo na mashirika hayo jijini New York, Marekani na Geneva, Uswisi , wanahamasisha mama aendelee kunyonyesha mtoto hata wakati wa janga la COVID-19, hata kama amethibitishwa kuwa na virusi vya Corona au anashukiwa kuwa navyo.

 Mashirika hayo yamesema kuwa, “wakati watafiti wanaendelea kuchunguza maziwa kutoka kwa mama mwenye virusi vya Corona au anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona, ushahidi wa sasa unadokeza kuwa hakuna uwezekano wa virusi hivyo kuambukizwa kupitia unyonyeshaji au kwa kumpatia mtoto maziwa yaliyokamuliwa kutoka kwa mama mwenye virusi au anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona.”

 Ripoti inasema kuwa uchunguzi kutoka mataifa 194, umebaini kuwa ni nchi 6 tu ambazo zina mikakati ya kisheria kuhusiana na kanuni ya kimataifa ya kutangaza maziwa mbadala ya mama na tatizo kubwa ni pale baadhi ya vituo vya afya vina matangazo ya maziwa ya kopo.

Akizungumzia ripoti hiyo, Dkt. Francesco Branca ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Lishe na Usalama wa Chakula, WHO, amesema kuwa, “mikakati mizito ya matangazo ya maziwa ya unga kwa mtoto, hasa kupitia wataalam wa afya ya kwamba wazazi waamini ushauri wa lishe na afya, ni pigo kubwa katika kuimarisha afya yam toto mchanga na mtoto kwa ujumla duniani kote.”

 Ripoti inasema kuwa mama aliyethibitishwa kuwa na virusi vya Corona au anayeshukiwa kuwa na virusi hivyo anaweza kuendelea kunyonyesha na kwamba wanapaswa kuzingatia kanuni za usafi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia maji na sabuni au dawa za kutakasa mikono kabla ya kumbeba au kumshika mtoto.

Audio Duration
2'8"
Photo Credit
UN