Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulemavu alio nao mtoto huyu haukumzuia kusaka kipato kwa ajili ya familia yake

Ulemavu alio nao mtoto huyu haukumzuia kusaka kipato kwa ajili ya familia yake

Pakua

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, athari za janga la virusi vya Corona au COVID-19 zimekuwa mbayá zaidi kwa watoto wenye ulemavu, ambapo mtoto mmoja mkazi wa mji mkuu Kinshasa, ambaye ni kiziwi, amelazimika kusaka mbinu za kuweza kupata kipato ili kusaidia familia yake. John Kibego na maelezo zaidi.

Kinshasa, mji mkuu wa DR Congo katika video hii ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF yenye lengo la kuangazia sauti za vijana katikati ya janga la COVID-19, anaonekana Steve Okito, mtoto mwenye umri wa miaka 14.

Yeye anaishi jijini kinshasa na mama yake na wadogo zake watatu wa kiume.

Steve ni mwanafunzi wa darasa la 7, lakini sasa hawezi tena kwenda shule na akizungumza kwa lugha ya alama  anasema kuwa, "shule zimefungwa kwa sababu ya janga la virusi vya Corona. Siwezi tena kuwaona marafiki zangu.”

Mtoto huyu anatoka familia maskini, na mama yake amepooza kwa hiyo analazimika kusaka kazi na kile afanyacho ni kusafisha magari jijini Kinshasa ili apate ujira.

Steve anasema kuwa, “Sasa hivi naosha magari kwa sababu shule imefungwa. Kila kitu kimefungwa na ninalazimika kupata fedha ili nitunze familia Fedha nampatia mama yangu. Hapa kwa mfano nimeosha hili gari na nimepata faranga 3000 sawa na dola 2. Lakini inategemea na mmiliki, wakati mwingine naweza kupata malipo ya juu zaidi.”

Ujio wa janga la Corona umefanya maisha ya Steve kuwa magumu zaidi kwa sababu hali ni ngumu zaidi kwa yeye kupata fedha akisema kuwa, "Kabla ya Corona, magari ya kuosha yalikuwa ni mengi, lakini sasa kila kitu kimefungwa, hakuna mtu anayewasha gari kwenda kutembelea rafiki au kuzunguka tu.”

Matarajio ya Steve ni kuwa shule zitafunguliwa ili aweze kuwaona tena rafiki zake,   shule zimefungwa kwa sababu ya COVID-19.

Hata hivyo Wizara ya afya ya DRC, UNICEF na wadau wanaendelea kushirikiana ili kuwepo kwa wafanyakazi wa kuwapatia watoto kama Steve msaada wa kisaikolojia ili waweze kuhimili madhara ya muda mfupi na muda mrefu ya janga la COVID-19.

Audio Credit
Anold Kayanda/John Kibego
Sauti
1'58"
Photo Credit
UNICEF VIDEO