Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Bangladeshi watu milioni 2.4 wahamishiwa kwenye makazi ya muda kufuatia kimbunga Amphan

Nchini Bangladeshi watu milioni 2.4 wahamishiwa kwenye makazi ya muda kufuatia kimbunga Amphan

Pakua

Kufuatia kimbunga Amphan kilichotua nchini Bangladesh wiki hii , wilaya 19 zimeathirika na watu zaidi ya milioni 2.4 wamelazimika kuhamishiwa kwenye makazi ya muda limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP. Flora Nducha na taarifa zaidi

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa njia ya mtandao mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa WFP Elisabeth Byrs amesema hamishwa hiyo imehusiha pia mifugo 500 na watu na mifugo yao wamewekwa kwenye makazi ya muda 12,000 ya waathirika wa kimbunga yaliyotengwa na serikali ya Bangladesh na kwamba timu ya WFP inafanya tathimini ya haraka ya mahitaji. 

Ingawa asilimia kubwa ya mazao yameshavunwa ripoti za awali zinaashiria kuwa kuna uharibifu mkubwa katika sekta ya uvuvi na hasa kwa wakulima wadogo wa dogo wa uduvi.

Ameongeza kuwa “WFP imeshaweka tayari chakula cha akiba zikiwemo biskuti za kuongeza nguvu kwa ajili ya familia 90,000 kwenye maeneo yaliyathirika na akiba zaidi ya chakula itakuwa tayari kugawanywa itakapohitajika. Na katika kupunguza athari za kusambaa maambukizi ya corona mamlaka imetenga vyumba tofauti kwa watu walio na dalili za COVID-19 na vituo vya kunawa mikono katika malazi hayo ya waathirika wa kimbunga.”

WFP imesema kimbunga cha sasa na msimu wa Monsoon unaokaribia vinaongeza hatari kwani mvua kubwa zinatishia kutawanya familia nyingi.

Kwa upande wa makambi ya wakimbizi wa Rohingya shirika hilo limesema hayakuathirika san ana kimbunga Amphan hata hivyo athari za moja kwa moja za kimbunga zinaweza kuwa mbaya sana kwa wakimbizi.

Bangladesh inakabiliwa na ongezeko la idadi ya wangonjwa wa COVID-19 na athari zake zinatishia kugeuza maendeleo yaliyopatikana kwa Zaidi ya miongo mitano amesema Bi. Byrs na kuongeza kwamba “Hali inachochewa na makambi ya wakimbizi wa Rohingya ya Cox’s Bazar ambako mazingira yanafanya kuwa vigumu watu kujitenga”

Amesema hatua za watu kusalia majumbani na vikwazo vingine vimeathiri maisha ya mamilioni ya watu Bangladesh nchi ambayo tayari watu milioni 40 wanaishi katika umasikini.

“Virusi vya COVID-19vinakatili Maisha ya watu lakini njaa pia inaweza kukatili Maisha, ili kuhakikisha walio hatarini Zaidi hawaachwi nyuma katika mapambano dhidi ya COVID-19, WFP inahitaji haraka dola milioni 200 kwa ajili ya hatua zake za kupambana na COVID-19 Bangladesh.” amesema Bi. Byrs.

 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'28"
Photo Credit
OCHA