Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Janga la COVID-19 ni kengele ya kutuamsha sote

Guterres: Janga la COVID-19 ni kengele ya kutuamsha sote

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema janga la virusi vya corona ni kengele ya kutuamsha sote hivyo ni wakati wa kushikamana na kusaka kinga na tiba ya kuutokomeza ugonjwa huu unaoiyumbisha dunia. John Kibego na taarifa zaidi

Antonio Guterres ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa Baraza la afya Duniani linalofanyika kwa njia ya mtandao Geneva Uswisi akiongeza kuwa “janga hili limedhihirisha udhaifu wa dunia, licha ya utaalam wa kisayansi na maendeleo ya teknolojia yaliyopatikana katika miongo ya karibuni virusi hivi vimetuadabisha. Hadi sasa hatujui jinsi gani ya kuvitokomeza, kuvitibu au chanjo ya kujikinga navyo na hatujui lini tunaweza kufanya haya.”


Katibu mkuu amesisitiza kwamba hata hivyo udhaifu ulioanikwa na COVID-19 sio tu kwamba umeathiri mifumo ya afya bali kila nyanja ya maisha, duniani kote na taasisi zote.


Ameliambia Baraza hilo la Afya kwamba udhaifu wa kuratibu juhudi za kimataifa kupambana na janga hili umewekwa wazi kama dunia ilivyoshindwa katika juhudi zingine za kimataifa ikiwemo vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, kudhibiti uzalishaji wa nyuklia, kukomesha uhalifu wa mtandaoni kwani vita vya mtandao tayari vimeshaanza na kutozingata sheria za kimataifa katika kulinda mazingira.


Guterres amesema, "huu ni wakati wa kuamka na kukomesha ukiritimba huu , hisia zetu za kutoweza kufanya lolote zituelekeze kwenye unyenyekevu mkubwa, vitisho vya kimataifa vinahitaji umoja mpya na mshikamano.”


Katibu Mkuu amewapongeza wote walio katika msitari wa mbele kupambana na janga hili la COVID-19 kuanzia waugunzi na wakunga, hadi wafanyakazi wa maabara, wasimamizi na mamilioni ya wahudumu wa afya kote duniani ambao amesema wanaweka rehani Maisha yao ili kuokoa ya wengine.


Amewaambia washirika wa Baraza hilo kwamba Umoja wa Mataifa unaendelea kusimama na maelfu ya wafanyakazi wa shirika la afya duniani WHO ambao wanafanyakazi usiku na mchana kote duniani kuzisaidia nchi wanachama kuokoa maisha na kuwalinda walio hatarini, kutoa muongozo, mafunzo na vipimo muhimu, matibabu na vifaa vya kujikinga.


“WHO haina mbadala , inahitaji kuongezewa rasilimali ili liweze kutoa msaada hususan kwa nchi zinazoendelea ambazo zinapaswa kuwa hofu yetu kubwa. Tuna tungu kama udhaifu wa mifumo ya kiafya. Kuzisaidia nchi zinazoendelea sio suala la hisani au ukarimu bali ni suala la kuimarisha maslahi yetu. Mataifa ya Kaskazini  hayawezi kulishinda janga la COVID-19 hadi pale mataifa ya Kuisni yatakapolishinda kwa wakati mmoja.”


Ameikumbusha dunia kwamba huu si wakati wa kutupiana lawama na kunyoosheana vidole bali “ni wakati wa umoja kwa jumuiya ya kimataifa kufanyakazi pamoja kwa mshikamano kukomesha virusi hivi na athari zake”


Ameongeza kuwa dunia haiwezi kutafakari mustakbali ulioghubikwa na hofu na mashaka ni ama ilishinde janga hili kwa Pamoja au ishindwe.


Baraza hio la 73 la Afya Duniani lililoandaliwa na WHO mwaka huu linajikika na janga la COVID-19 na linashirikisha nchi zote wanachama 194. Litakunja jamvi Mei 21.


 

 

Audio Credit
John Kibego
Sauti
2'55"
Photo Credit
UN Photo/Manuel Elías