Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msiwe na hofu ya kuchangia damu wakati huu wa COVID-19, bado tunahitaji kuokoa maisha

Msiwe na hofu ya kuchangia damu wakati huu wa COVID-19, bado tunahitaji kuokoa maisha

Pakua

Kitengo cha damu salama katika hospitali ya rufaa mkoa wa Dodoma nchini Tanzania kimewatoa hofu wachangiaji wa damu kuwa uwepo wa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 usiwatishe kwenda kuchangia damu kwani hawawezi kuambukizwa wala kuwaambukiza wengine kwa kuchangia damu. Devotha Songorwa na taarifa zaidi

Msimamizi  wa kitengo hicho Dkt. Leah Kitundya anasema kwa sasa kiwango cha uchangiaji wa damu kimepungua kwa sababu wachangiaji wakubwa ni wanafunzi wa sekondari na vyuo ambao wamerudi nyumbani baada ya masomo kusitishwa  kwa lengo la kuepuka msongamano  unaoweza kuchangia maambukizi mapya ya virusi hivyo wakishirikiana na wanajeshi.
 
Dkt.  Leah akaongeza kuwa changamoto ya virusi vya Corona vimeathiri kwa kiasi kikubwa uchangiaji wa damu na kusababisha kutofikia lengo walilojiwekea  la kila mwezi kukusanya chupa 1000 hadi 1500 lakini sasa hali imekuwa tofauti ambapo kwa mwezi uliopita wamekusanya chupa 500 akisema kuwa mwitiko wa wananchi kujitokeza kuchangia ni mdogo.
 
Pia msimamizi huyo akatoa ufafanuzi juu ya malalamiko ambayo hutolewa na baadhi ya watu kuwa wamekuwa wakitozwa fedha kupata damu kwa ajili ya wagonjwa wao akiongeza kuwa kundi la watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika zoezi la uchangiaji wa damu ili kuokoa maisha ya watu.
Dkt. Leah anaeleza tahadhari wanazochukuwa wakati wa uchangiaji wa damu katiki kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona na hatua ambazo huchukua wanapobaini kuwa damu hiyo si salama kwa matumizi.
 
 
 

Audio Credit
Devotha Songorwa
Sauti
2'13"
Photo Credit
UNFPA