Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF:COVID-19 kusababisha nyongeza ya watoto 6,000 kufariki dunia kila siku

UNICEF:COVID-19 kusababisha nyongeza ya watoto 6,000 kufariki dunia kila siku

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wiki hii linazindua kampeni iitwayo #Reimagine, yenye lengo la kuzuia janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, lisiwe janga la kudumu hususan kwa watoto walio hatarini zaidi kutokana na umaskini, kutengwa au ghasia majumbani. Ahimidiwe Olotu na taarifa zaidi

Kampeni hiyo inazinduliwa wakati huu ambapo utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Lancet, umebaini kuwa janga la Corona litaongeza vifo vingine vya watoto 6,000 kila siku kwa miezi sita ijayo, vifo vitakavyosababishwa na magonjwa yanayozuilika.
 
Taarifa ya UNICEF iliyotolewa hii leo mjini New York, Marekani inasema kuwa hali hiyo ni dhahiri kwa sababu, “janga la COVID-19 linaendelea kudhoofisha mifumo ya afya na kuvuruga taratibu za huduma za afya.”
 
Vifo hivyo 6,000 kila siku kwa mujibu wa UNICEF ni nyongeza kwenye vifo vya watoto milioni 2.5 ambao hufariki dunia katika kipindi cha miezi 6 kwenye nchi 118 kabla ya kutimiza umri wa miaka 5.
 
“Hii inatishia mafanikio yaliyopatikana katika kuzuia vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5,”  imesema UNICEF ikiongeza kuwa wazazi 567,000 nao watapoteza maisha katika kipindi cha miezi 6, ikiwa ni nyongeza ya wale 1,144,000 waliofariki dunia katika nchi hizo 118.
 
COVID-19 imevuruga ratiba za huduma za afya kutokana na amri za kutotembea hovyo, watu kuzuiliwa majumbani, kusitishwa kwa njia za usafirishaji na pia kwa hofu ya jamii kuogopa maambukizi.
 
Utafiti huo uligawa makundi matatu ya mazingira ya madhara ya COVID-19, kuanzia hali mbaya zaidi, hali mbaya kidogo na hali mbaya.
 
Je taifa lako ni miongoni mwa yatakayokuwa na vifo vingi zaidi vya watoto?
 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mazingira mabaya zaid, nchi 10 zinazoweza kuwa na nyongeza kubwa zaidi ya vifo vya watoto ni Bangladesh, Brazil, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, India, Indonesia, Nigeria, Pakistan, Uganda 
na Tanzania.
 
Nchi 10 ambazo katika hali mbaya zaidi zinaweza kuwa na nyongeza kubwa zaidi ya vifo vya watoto ni Djibouti, Eswatini, Lesotho, Liberia, Mali, Malawi, Nigeria, Pakistan, Sierra Leone and Somalia.
 
UNICEF inataka serikali hizo zihakikishe kuna mwendelezo wa utoaji wa huduma za kuokoa maisha ya mama na mtoto.
 
Sasa nini kifanyike?
 
Ni kwa mantiki hiyo shirika hilo linazindua kampeni ya #Reimagine ambamo kwayo inatoa wito wa dharura kwa serikali, umma, wahisani na sekta binafsi ziungane na UNICEF kuchukua hatua, kuibuka na kufikiria upya dunia ambayo hivi sasa imeghubikwa na virusi vya Corona.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore, akinukuliwa kwenye taarifa ya shirika lake amesema kuwa, “COVID-19 ni janga la haki za mtoto. Tunapaswa kuchukua hatua fupi, za kati na za mrefu siyo tu katika kushughulikia changamoto zilizosababishwa na janga hili na madhara yake ya juu juu kwa mtoto, bali pia kuainisha mbinu sahihi za kujenga upya dunia bora zaidi pindi janga hili litakapomalizika.”
 
Bi. Fore amesema kwa hili kufanikiwa, “tunahitaji mawazo, rasilimali na moyo wa kila mtu. Ni wajibu wetu wa pamoja hii leo kutafakuri dunia itakuwa vipi kesho.”
 
 
 

 

Audio Credit
Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
2'3"
Photo Credit
© UNICEF/Till Muellenmeister