Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres:Tukihakikisha haki za wenye ulemavu, tunawekeza katika mustakbali wa Pamoja

Guterres:Tukihakikisha haki za wenye ulemavu, tunawekeza katika mustakbali wa Pamoja

Pakua

Katika mazingira ya kawaida watu wenye ulemavu mara nyingi hukosa fursa ya huduma za msingi kama vile elimu, huduma za afya na fursa za kiuchumi au ushiriki katika jamii.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika uzinduzi wa sera kuhusu watu wenye ulemavu na janga la corona au COVID-19.

Katika uzinduzi huo Bwana Guteres amesema janga la COVID 19 linaathiri kila nyanja ya jamii zetu na leo hii anaelezea jinsi gani janga hili linavyoathiri watu bilioni moja wenye ulemavu duniani.

"Janga hili linaongeza hali ya kutokuwepo usawa na kutoa vitisho vipya. Watu wenye ulemavu ni miongoni mwa walioathirika vibaya na mgogoro huu katika upande wa vifo.”

Amesisitiza kwamba ni lazima tuhakikishe haki sawa za watu wenye ulemavu katika fursa za kupata huduma za afya na mipango ya kuokoa maisha wakati wa janga hili.

Ameongeza kuwa watu wenye ulemavu waliokuwa wakikabiliwa na ubaguzi kabla ya janga la COVID-19 sasa wako katika hatari  ya kubaguliwa zaidi na hata kupoteza ajira zao, hivyo ametoa wito wa kuchukuliwa hatua akisema

“Nazitaka serikali kuwaweka watu wenye ulemavu katikati ya hatua za kukabiliana na kujikwamua na janga la COVID-19, kujadiliana nao na kuwahusisha. Tutakapo hakikisha haki za watu wenye ulemavu, tunawekeza katika mustakbali wetu wa pamoja.”

Audio Credit
John Kibego
Audio Duration
1'25"
Photo Credit
UNICEF/Rebecca Vassie