Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni lazima tuilinde sayari dunia na watu wake-Guterres

Ni lazima tuilinde sayari dunia na watu wake-Guterres

Pakua

Janga la mlipuko wa virusi vya corona au COVID-19 limefanya macho yote ya Dunia kuelekezwa kwenye mtihani huu mkubwa zaidi ambao ulimwengu umekumbana nao tangu Vita vya Pili vya  Dunia amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Antonio Guterres katika ujumbe wake maalum wa siku ya kimataifa ya mama sayari Dunia hii leo amesema

Ni lazima tufanye kazi pamoja kuokoa maisha, kupunguza madhila, na kupunguza madhara ya kiuchumi na kijamii kwani athari za virusi vya corona ni za sasa na za kutisha.”

Guterres amesema mbali ya COVID-19 kuna janga jingine kubwa ambalo ni tatizo linaloikumba sayari Dunia kimazingira. “Bayoanuwai inaendelea kudorora, mabadiliko ya tabianchi yanafikia kiwango kisichoweza kudhibitika. Ni lazima tuchukue hatua kabambe za kuilinda sayari yetu kutokana na virusi vya corona na tishio la mabadiliko ya tabianchi.”

Ameongeza kuwa janga la sasa ni kengle ya kutuamsha kufanya mabadiliko , kutojikweza na kutumia fursa kufanya mambo vyema zaidi kwa siku zijazo.

Mawio katika jimbo la Carchi nchini Ecuador (Septemba 2018)
WMO/Boris Palma
Mawio katika jimbo la Carchi nchini Ecuador (Septemba 2018)

 

 Kwa mantiki hiyo amependekeza hatua sita zinazohusiana na tabianchi, kama mwongozo wa kujikwwamua na kazi tunayopaswa kufanya.

 “Mosi tunapotumia kiasi kikubwa cha fedha kujikwamua kutokana na virusi vya corona, ni lazima tufungue fursa mpya za ajira na biashara kwa hali ya mpito isiyo chafuzi, Pili panapotumiwa fedha za walipa ushuru kukwamua biashara, pazingatiwe upatikanaji wa ajira zinazojali mazingira na ukuaji endelevu.”

Zingine amezitaka kuwa “Tatu nguvu za kifedha zitumiwe kubadili uchumi kuwa unaojali mazingira, na kuzifanya jamii na watu kuwa jasiri zaidi. Nne fedha za umma zitumiwe kuwekeza kwa mustakabali, sio zama, na ziende kwa sekta na miradi endelevu inayosaidia mazingira na tabianchi, ruzuku ya mafuta ya kisukuku lazima ikomeshwe na wachafuzi  waanze kubeba gharama ya uchafuzi wao. Tano matishio ya tabianchi na fursa ni lazima vijumuishwe kwenye mifumo ya fedha, pamoja na nyanja zote za sera za umma na miundombinu. Na sita tunapaswa kufanya kazi pamoja kama jamii ya kimataifa. “

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba kanuni hizi sita ni mwongozo muhimu wa kujikwamua vyema zaidi pamoja. Gesi chafuzi, kama virusi, haziheshimu mipaka ya nchi. “ Na kwenye siku hii ya Mama Sayari Dunia, ungana nami kutaka mustakabali mwema kwa watu na sayari.”

 

Audio Credit
UN News/ Assumpta Massoi
Sauti
2'21"
Photo Credit
UN News/Laura Quinones