Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matangazo ya elimu kwa televisheni na mtandaoni yasaidia wakimbizi Jordan

Matangazo ya elimu kwa televisheni na mtandaoni yasaidia wakimbizi Jordan

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa kushirikiana na serikali ya Jordan, wamechukua hatua hatua kuhakikisha kuwa wakimbizi wa Syria katika kambi ya Za’atari nchini humo wanaendelea na masomo licha ya kufungwa kwa shule 32 kambini humo kutokana na hofu ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Kambini Zaatari, kambi kubwa zaidi ya wakimbizi eneo la Mashariki ya Kati, ni ndani ya familia moja ya baba na watoto wake 6 ambao wote ni wanafunzi.

Kambini hapa wanafunzi elfu 18 kuanzia wale wa chekechea hadi sekondari wamesajiliwa kupata mafunzo wakiwa nyumbani kutokana na hofu ya virusi vya Corona au COVID-19.

Miongoni mwao ni Raghad na Rani wakielekezwa na baba yao!

Raghad anasema kuwa kupitia masomo ya televisheni na makundi ya shule kupitia kwenye simu wanaweza kuendelea na masomo.

Wanajifunza kuchora, kusoma na kuandika wakitumia televisheni na simu ya baba yao ambaye anasema,

“Nina watoto 6 ambao wanatumia simu moja kuwasiliana na makundi yao. Najaribu kutenga muda kwa kila mmoja kuungana na kundi lake, hii ina maana kwamba, wakati mwingine kuna kuchelewa katika kujibu maswali yanayotumwa na mwalimu kwenye kundi.”

Kwa ndugu zao wakubwa, Ahmed na Ayman, mambo ni murua ambapo Ayman anasema kuwa,

“Ni sawa na shule ya kawaida. Hakuna kilichobadilika. Tofauti kubwa ni kwamba darasani unamuona mwalimu lakini sasa unamuona mtandaoni au kupitia televisheni.”

Ili kuweza kukidhi mahitaji ya familia zilizosalia nyumbani kila siku, UNHCR na mamlaka za kambi, wameongeza usambazaji wa umeme katika kila kaya kutoka saa 8 hadi 12 kwa siku.

Baadaye wiki hii, UNHCR na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wanatarajiwa kutoa taarifa ya pamoja kutoa wito wa usaidizi zaidi kwa ulinzi, huduma ya afya na elimu kwa watoto wakimbizi duniani kote, ili janga la COVID-19 lisitoweshe mafanikio ya awali yaliyopatikana kwa mbinde.

TAGS: UNHCR, Za’atari, Jordan, Syria

 

Audio Duration
2'17"
Photo Credit
UN News