Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Imarisha afya ya mama na mtoto ni mkombozi wa wajawazito Kenya

Imarisha afya ya mama na mtoto ni mkombozi wa wajawazito Kenya

Pakua

Nchini Kenya mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF uitwao Imarisha Afya ya Mama na Mtoto umesaidia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa mama kuhudhuria kliniki sambamba na kupata lishe bora wakati wa ujauzito.

Mradi huo unaotekelezwa katika kaunti ya Kakamega nchini Kenya kwa ufadhili wa ubalozi wa Sweden nchini humo, unawezesha kusambazwa kwa taarifa na kupatia kaya maskini fedha za kupunguza vikwazo vya kiuchumi, kijamii na kitamaduni vya kupatikana kwa huduma za afya na lishe.

Lilian Abuoro ambaye ni mfanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa akifanya kazi na UNICEF kama afisa wa ulinzi anasema kuwa, “tunapatia kaya shilingi Elfu 12 za Kenya sawa na dola 120 za kimarekani kwa kipindi cha miaka 2 ambayo ni kabla na baada ya kujifungua. Fedha hizi kimsinngi hutumika kwa usafiri na pia kuboresha lishe kwa wajawazito kununua matunda na mboga mboga na kujumuisha kwenye mlo.”

Mwanaisha Mapesa, ni mkazi wa Kakamega ambaye amenufaika na mpango huo. Yeye ni mama wa watoto wanne ambapo watatu alijifungulia nyumbani kwa msaada wa mkunga wa jadi lakini mtoto wa nne alikwenda hospitali.

Bi. Mapesa anasema kuwa, “ukienda hospitali wanakufanyia uchunguzi waone vile unavyoendelea na mtoto anavyoendelea.”

Ili kufuatilia kuwa wanufaika wa mradi wa Imarisha Afya ya Mama na Mtoto wanafuata kanuni, UNICEF imeweka utaratibu huo ambapo Cynithia Waswa karani wa mradi huo kaunti ya Kakamega anasema kuwa, “kila mara wakishatoka kliniki, muuguzi anawaagiza wafike hapa ili wasajili taarifa zao. Iwapo wanafanya hivyo ndipo wanaweza kupatiwa fedha alimradi wawe wamethibitishwa na kamati ya wahudumu wa afya ya uidhinishaji kuwa ni kaya yenye mahitaji na hii ni kaya yenye kipato cha chini ya dola moja kwa siku.”

Lilian ambaye ameamua kujitolea kufanya kazi ya kuelimisha wanawake na wajawazito umuhimu wa kujifungulia hospitali baada ya rafiki yake mmoja kufariki dunia wakati wa kujifungua anasema kuwa sasa anatumia ufahamu wake kuelimisha wanawake kuanza kliniki pindi tu wanapobaini kuwa wana ujauzito kwa sababu hata kama ana tatizo linaweze kushughulikiwa kwenye kituo cha afya.

Halikadhalika anasema kuwa, “nimegundua kuwa akina mama wengi bila kujali kisomo chao au umaskini wao wanaweza kufanya uamuzi mzuri pindi linapokuja suala la afya zao iwapo wana taarifa sahihi. Kwa hiyo ndio maana tumekuwa tunafanya kazi kusambaza taarifa na baada ya hapo inakuwa rahisi kwa wao wenyewe kusaka huduma hizo wakishakuwa na taarifa, hivyo kupunguza pengo la ufahamu. Mradi Imarisha Afya ya Mama na Mtoto ni muhimu kwa sababu, ni njia fanisi ya kupunguza vifo vya wanawake wajawazito,

Takwimu za UNICEF zinaonesha kuwa nchini Kenya, wajawazito 342 hufariki dunia katika kila wajawazito 100,000 wanaojifungua.

TAGS: Kenya, UNICEF, Kakamega, Sweden

Audio Credit
UN News/Assumpta Massoi
Audio Duration
1'44"
Photo Credit
UNFPA Mozambique