Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Si wakati wa kupunguza rasilimali kwa shirika lolote lile la kibinadamu linalopambana na COVID-19-Guterres

Si wakati wa kupunguza rasilimali kwa shirika lolote lile la kibinadamu linalopambana na COVID-19-Guterres

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema huu si wakati wa kupunguza rasilimali za kufanikisha operesheni za shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO. Grace Kaneiya na ripoti kamili.
 
(Taarifa ya Grace Kaneiya)
 
Bwana Guterres amesema hayo katika taarifa iliyotolewa Jumanne usiku na msemaji wake jijini New York, Marekani akisema kuwa siyo tu kwa WHO bali pia si wakati wa kupunguza rasilimali kwa shirika lolote lile la kibinadamu linalopambana hivi sasa na ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19.
 
Kauli ya Katibu Mkuu imekuja saa chache kufuatia tangazo la leo Jumanne la Rais wa Marekani Donald Trump la kusitisha fedha kwa WHO, hadi baada ya tathmini ya hatua za shirika hilo dhidi ya mlipuko wa COVID-19.
 
Katibu Mkuu amerejelea kauli yake ya tarehe 8 mwezi huu ya kwamba janga la COVID-19 ni moja ya changamoto kubwa kuwahi kukumba dunia na ni janga kubwa zaidi la kibinadamu lenye madhara makubwa kijamii na kiuchumi.
 
Amesema maelfu ya wafanyakazi wa WHO wako  mstari wa mbele wakisaidia nchi wanachama na wananchi wao hususan walio hatarini zaidi, wakiwapatia mafunzo, mwongozo, vifaa na huduma muhimu za kuokoa maisha huku wakikabiliana na virusi.
 
 
(sauti ya Antonio Guterres)
 
“Wapendwa janga hili linarejesha nyumbani umoja wetu ambao ni muhimu katika familia ya ubinadamu wetu. Kuzuia kuenea zaidi kwa COVID-19 ni jukumu letu zote kwa pamoja. Umoja wa Mataifa likiwemo shirika la afya duniani umejipanga kikamilifu.Kama sehemu ya familia yetu ya kibinadamu tunafanya kazi saa 24 siku 7 kwa wiki na serikali ili kutoa muongozo wa kimataifa kuusaidia ulimwengu kuchukua hatua za kukabili tishio hili.”
 
Guterres amesema ni kwa imani yake kuwa WHO inapaswa kuungwa mkono kwa sababu bila shaka ni muhimu sana katika juhudi za dunia za kupambana na COVID-19.
 
Amesisitiza kuwa huu ni wakati wa mshikamano na wakati wa umoja na jamii ya kimataifa kushirikiana na kukomesha hivi virusi na madhara yake.

 

Audio Credit
Flora Nducha/ Grace Kaneiya
Audio Duration
2'2"
Photo Credit
UN Photo/Evan Schneider