Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

9 Aprili 2020

9 Aprili 2020

Pakua

Assumpta Massoi : Hujambo na Karibu kusikiliza Jarida kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, kutoka hapa New York Marekani.

JINGLE (04”)

ASSUMPTA:Ni Alhamisi  09 Aprili mwaka 2020, mwenyeji wako studioni hii leo ni mimi ASSUMPTA MASSOI

1: Kitabu cha watoto chazinduliwa kuwaelimisha kuhusu COVID-19
Zaidi ya mashirika 50 ya kibinadamu yakiwemo yale ya Umoja wa Mataifa yameandaa kitabu kipya cha kusaidia watoto kuelewa na kufahamu kwa kina ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19. Grace Kaneiya na ripoti kamili.
(Taarifa ya Grace Kaneiya)
Kitabu hicho kilichopatiwa jina Shujaa wangu ni wewe na kikiwa na kurasa 22, mhusika wake mkuu ni kikaragosi cha kufikirika kiitwacho Ario.
Katika simulizi hiyo ya kusisimua, Ario anamtokea mtoto Sarah ndotoni na anamchukua na kusafiri pamoja mabara mbalimbali ambako wanakutana na watoto wenye shaka na shuku kuhusu ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.
Mathalani simulizi inawafikisha eneo lenye mapiramidi ambako mtoto Salem anawajulisha kuwa wasisogeleane kutokana na virusi vya Corona na ndipo wanajadili suala la kunawa mikono, hatua ambayo ni muhimu kwa ajili ya kujikinga na kukinga wengine dhidi ya virusi vya Corona.
Walengwa wa kitabu hiki ni watoto wenye umri wa kuanzia miaka 6 hadi 11 na ni mradi wa kamati ya mashirika mbalimbali kuhusu afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia katika mazingira ya dharura.
Mwanzoni mwa maandalizi ya kitabu hicho, zaidi ya watu 17000 wakiwemo watoto, wazazi, walezi na walimu kutoka kona mbalimbali duniani walielezea jinsi gani wanakabiliana na janga la COVID-19.
Michango  yao ilikuwa muhimu kwa mwandishi wa kitabu na mchoraji Helen Patuck na timu nzima katika kuhakikisha simulizi na ujumbe vinaendana na watoto wa hali tofauti na maeneo mbalimbali duniani.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la afya, WHO, la kuhudumia watoto, UNICEF, la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO na wadau wao likiwemo Save the Children na shirikisho la vyama vya  nyekundu na hilal nyekundu.
Akizungumzia kitabu hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore, amesema kuwa duniani kote, maisha ya watoto yamebadilika, wengi wao katika nchi zenye karantini na hivyo, “kitabu hiki kitasaidia watoto kuelewa na kukabiliana na hali ya sasa na kujifunza ni kwa vipi wanaweza kuchukua hatua ndogo tu na kuwa mashujaa katika simulizi zao.”
Ili kuhakikisha kitabu hicho kinafikia watoto wengi kadri iwezekanavyo, kitatafsiriwa kwa lugha nyingi, ambapo leo kitabu hicho kitazinduliwa kikiwa katika lugha 6 huku nyingine 30 zikiwa kwenye maandalizi. 
===================================================

2: UNHCR yajipanga mapema kudhibiti COVID-19 katika kambi za wakimbizi wa Rohingya 
 
Pamoja na kuwa hakuna mgonjwa yeyote wa virusi vya corona, COVID-19 ambaye ameripotiwa miongoni mwa wakimbizi nchini Bangladesh, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linachukua hatua za kujiandaa kukabiliana na mlipuko ikiwemo kujenga wodi za kuwatibu wagonjwa katika maeneo hayo. Taarifa zaidi na John Kibego.
 
(Taarifa ya John Kibego)
 
Ni katika kambi ya wakimbizi ya Kutupalong nchini Bangladesh, wafanyazi wajenzi wako katika harakati za kukimbizana na muda, wengine wanafunga mianzi na wengine wanachanganya mchanga. 
 
Mwakilishi wa UNHCR nchini Bangladesh Steven Corliss anazungumza na maafisa wa UNHCR na pia wafanyakazi wanaofanya kazi katika eneo la ujenzi. Kisha anasema,
 
(Sauti ya Steven Corliss)
 
“mpaka sasa, ni kama tumekuwa na bahati hakuna mgonjwa wa COVID-19 katika makazi ya wakimbizi wa Rohingya kusini mwa Bangladesh lakini tuko katika mbio dhidi ya muda. Tunajaribu kuwa tayari, unaona nyuma yangu kuna kituo cha kuwatenga na kuwatibu wagonjwa ambacho kinaweza kutoa huduma ya haraka kwa watu 150 hadi 200.”
 
Bwana Corliss anasema pia kuwa miundobinu hiyo inajengwa  ili iwahudumie wakimbizi wa Rohingya na jamii wenyeji katika wilaya ya Cox’s Bazar,
 
(Sauti ya Steven Corliss)
 
“vituo kama hivyo vinajengwa katika maeneo tofauti ndani na pia maeneo karibu na makazi ya wakimbizi wa Rohingya. Vituo hivyo vitawahudumia wakimbizi lakini vitawahudumia jamii za wenyeji. Hii ni muhimu, virusi haviangalii hadhi yako, haijalishi kama wewe ni mrohingya au mbangladeshi kwa hivyo kila kitu tunachokifanya, kila hatua zetu lazima ziwe kwa ajili ya jamii zote mbili. Umoja wa Mataifa na wadau wetu mashirika yasiyo ya kiserikali wanafanya kazi kwa ukaribu sana na serikali kuhkikisha kuwa kunakuwa na mipango hiyo.”
 
Serikali ya Bangladeshi, ikiongoza katika mapambano dhidi ya COVID-19, imeweka mpango wa kitaifa ambao unawazingatia wakimbizi. Jumuiya ya misaada ya kibinadamu inaendelea kuhakikisha kuwa wakimbizi wanajumuishwa ipasavyo katika kutekeleza mipango hii na kumefanyika mafunzo ya kukinga ugonjwa kwa wafanyakazi wa sekta ya afya na pia uhamasishaji wa utaratibu wa kujisafi.
====================================================
STUDIO. MIDWAYSTING
====================================================
ASSUMPTA: Na punde ni makala ambapo leo tunaelekea nchini Tanzania kusikia kuhusu mpango wa kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona hospitali ya taifa ya Muhimbili.
====================================================

3: Ni wajibu wetu kuwalinda wakimbizi dhidi ya COVID-19-UNHCR 
 
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linachukua tahadhari zote na kufanya kila liwezalo ili kuwalinda dhidi ya janga la virusi vya Corona, COVID-19 wakimbizi walio katika kambi mbalimbali za wakimbizi barani Afrika . Jason Nyakundi na taarifa zaidi
 
(TAARIFA YA JASON NYAKUNDI)
Nats…….
Katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini wakimbizi wakimbizi wakipangwa katika mistari maalum ubali wa mita moja wakisubiri kupayta mgao wa chakula huku wakipatiwa maelekezo maalum ya kujikinga na virusi vya Corona, COVID-19 na pia kupimwa joto la mwili.
Nats……….
Shirika hilo la wakimbizi linasema ingawa idadi ya wagonjwa walioripotiwa kuwa na virusi hivyo na kuthibitishwa barani Afrika ni ndogo, lakini zaidi ya asilimia 80 ya wakimbizi na karibu wakimbizi wote wa ndani wanaishi katika nchi za kipato cha chini na cha wastani nchi ambazo nyingi mifumo yake ya afya, maji, na mifumo ya usafi ni duni na wanahitaji msaada wa haraka.
Mbali ya kambi ya Kakuma Kenya kambi zingine ambako hatua madhubuti zinachukuliwa hivi sasa ni kambi ya Mtabila nchini Tanzania, kambi ya Nampula nchi Msumbiji, kambi ya wakimbizi wa ndani ya Juba Sudan kusini na kambi ya wakimbizi ya West Darfur nchini Sudan.
Natts….
Kwenye kambi ya Mtabila Kigoma Tanzania miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na UNHCR ni kuwanapatia wakimbizi elimu ya kunawa mikono kwa sababuni na kuzingatia usafi. Pia wanagawa sabauni hizo na kuongeza fursa ya upatikanaji wa maji.
Kwa nchi za Msumbiji, Sudan Kusini na Sudan pamoja na hatua kama hizi pia kutoa mafunzo kwa waelimishaji wa kijamii ambao watawafunza wakimbizi jinsi ya kujilinda na virusi hivyo.
Pamoja na kuchukua hatua zote hizo UNHCR iinazisaidia serikali katika hatua za kuzuia na huduma za afya za kukabiliana na COVID-19 ikiwa ni pamoja na kuwapa vifaa vya kitatibu na kuhakikisha taarifa muhimu kuhusu mlipuko huu zinapatikana na kuwafikia wakimbizi kwa urahisi.
Shirika hilo linasema linaendelea pia kutoa vifaa vya malazi na vifaa vingine muhimu pamoja na kuhakikisha kwamba haki za wakimbizi , wakimbizi wa ndani na watu waliolazimika kukimbia makwao zinaheshimiwa na kulindwa.

 
===================================================
STUDIO: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
ASSUMPTA: 
Na sasa ni makala tuungane na Stella Vuzo, Afisa wa Habari wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania akiwa amevinjari kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili kushuhudia mradi wa Mo Dewj Foundation wa kuweka sehemu mahsusi ya kunawa mikono  kwa ajili ya wageni wanaofika pale hospitaliani, mgeni wa leo anaanza kwa kujitambulisha
=================================================
STUDIO: PLAY MAKALA
====================================================

ASSUMPTA: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
ASSUMPTA:

Shukran Stella Vuzo kwa makala hiyo
====================================================
Na sasa ni mashinani, leo unamsikia Rebecca Kapaira, mama wa watoto watano nchini Zimbabwe, akielezea changamoto wanazokumbana nazo za kupata chakula kutoka shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa wakati huu wa COVID-19.
 ===================================================
Studio: Play Mashinani
====================================================
ASSUMPTA:
Shukrani sana  Rebecca Kapaira, kutoka Zimbabwe kwa ujumbe huo murua.
==================================================
STUDIO: Play Bridge

ASSUMPTA: Na hadi hapo natamatisha jarida letu la leo. Tupatane kesho kwa habari na makala kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa unaweza kupata matangazo na taarifa nyingine na kujifunza Kiswahili kwenye wavuti wetu news.un.org/sw. Msimamizi  wa matangazo ni GRACE KANEYA na fundi mitambo na mimi ASSUMPTA MASSOI, nasema kwaheri kutoka New York.

==================================================
TAPE: CLOSING BAND

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
12'40"