Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

7 Aprili 2020

7 Aprili 2020

Pakua

Assumpta Massoi : Hujambo na Karibu kusikiliza Jarida kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, kutoka hapa New York Marekani.

JINGLE (04”)

ASSUMPTA:Ni Jumanne 07 Aprili mwaka 2020, mwenyeji wako studioni hii leo ni mimi ASSUMPTA MASSOI

1: Tunahitaji kuwekeza haraka kuziba pengo la wauguzi duniani:WHO 
Mlipuko wa virusi vya Corona COVID-19 unadhidhirisa haja ya kuimarisha sekta ya wahudumu wa afya kote duniani , kwa mujibu wa ripoti mpya ya “hali ya wauguzi duniani 2020.”Flora Nducha na taarifa Zaidi
(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)
Ripoti hiyo iliyotolewa leo inatoa mtazamo wa kina kuhusu kundi kubwa la wafanyakazi wa huduma za afya.
Pia ripoti hiyo imebaini mapengo makubwa yaliyoko katika kundi hilo la wauguzi na maeneo ya kuyapa kipaumbele kama uwekezaji wa elimu kwa wauguzi, ajira na uongozi kuweza kuimarisha wauguzi kote duniani ili kuboresha afya kwa wote.
Waugunzi ni zaidi ya nusu ya wahudumu wote wa afya kwa mujibu wa ripoti hiyo na wanatoa huduma muhimu katika mfumo mzima wa afya.
“Kihistoria na hata ilivyo sasa wauguzi wako msitari wa mbele kupambana na milipuko ya magonjwa ambayo inatishia afya kote ulimwenguni. Duniani kote wanadhihirisha huruma yao, uhodari na ujasiri wakati wa napopambana na janga la COVID-19..”
Akisisitiza umuhimu wa kundi hili la wahudumu wa afya mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO, Dkt. Tedross Adhamon amesema”Wauguzi ni uti wa mgongo wa mfumo wowote wa afya. Leo wauguzi wengi wanajikuta wako msitari wa mbele katika mapambano dhidi ya COVID-19. Na ripoti hiini kumbusho la jukumu muhimu wanalolifanya na kusisitiza kuhakikisha kwamba wanapata msaada wanaouhitaji kuhakikisha dunia inakuwa na afya.”
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiunga mkono hoja hiyo ya umuhimu wa wauguzi amesema 
 
(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES- ARNOLD)
“wauguzi hubeba baadhi ya mizigo mkubwa kabisa ya huduma za afya. Wauguzi hufanya kazi ngumu na kwa saa nyingi, huku wakihatarisha kuumia, maambukizi na mzigo wa afya ya akili ambao unaambatana na kazi hiyo inayotia kiwewe. Mara nyingi hutoa faraja wakati wa mwisho wa maisha.”
 
Ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja na WHO kwa kushirikiana na baraza la kimataifa la wauguzi (ICN) na Nursing Now imeonyesha kwamba leo hii duniani kote kuna wauguzi takriban milioni 28 na zaidi ya asilimia 80 ya wauguzi wote duniani wanafanyakazi katika maeneo yaliyo na nusu ya watu wote wa dunia
 
Ili kuepuka pengo la kimataifa la wauguzi ripoti inakadiria kwamba nchi zinazokabiliwa na uhaba wa wauguzi zinatakiwa kuongeza idadi ya wauguzi wanaohitimu kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka sambamba na kuimarisha uwezo wa kuajiriwa na kusalia kwenye mifumo ya afya. 

Ujumbe wa ripoti hiyo uko bayana “serikali zinahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa kusomesha wauguzi , kuunda ajira za wauguzi na uongozi. Bila wauguzi, wakunga na wahudumu wengine wa afya nchi haziwezi kushinda vita dhidi ya magonjwa ya milipuko au kufikia huduma za afya kwa wote na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
===================================================

2: Fikra za kikoloni katika kujaribu chanjo ya COVID-19 Afrika zikome- WHO
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema ameshtushwa sana na kauli za wiki iliyopita kutoka kwa baadhi ya wanasayansi wakipendekeza kuwa majaribio ya kwanza ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 yatafanyikia Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi siku ya Jumatatu, Dkt, Tedros amesema,
(Sauti ya Dkt. Tedros)
“Kwa kweli nilishtushwa sana. Nikasema wakati huu ambapo tunataka mshikamano, kauli za kibaguzi kama hizo haziwezi kusaidia na ni kinyume na mshikamano. Afrika haiwezi na katu haitakuwa uwanja wa majaribio ya chanjo yoyote. Tutafuata kanuni zote kujaribu chanjo au dawa yoyote duniani kote,  kwa kutumia kanuni hiyo hiyo,  iwe ni Ulaya au Afrika au kwingineko, tutafuata kanuni hiyo na kama kuna umuhimu wa majaribio kwingineko kutibu binadamu, vivyo hivyo kwa usawa. Na  fikra za kikoloni sasa zikome na WHO katu haitoachia kitendo hicho kifanyike Afrika au kwingineko.”
Badala yake amesema taratibu sahihi za majaribio ya chanjo zitafuatwa na binadamu watatendewa kama binadamu kwa kuwa watu wote ni binadamu.
Ameongeza kuwa, ni jambo la kushangaza sana kauli kama hizo za kufanya majaribio ya chanjo ya COVID-19 Afrika zinatokana kwa wanasayansi katika karne hii ya 21 na wamelaani vikali.
====================================================
STUDIO. MIDWAYSTING
====================================================
ASSUMPTA: Punde ni makala ambapo tutakuwa nchini Kenya kuangazia ufafanuzi wa serikali kuhusu katazo la serikali la kutoingia katika baadhi ya miji ili kupambana na virusi vya corona.
====================================================

3: Jumuiya ya michezo yakabiliwa na changamoto kubwa sababu ya COVID-19 :UN
Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya michezo kwa maendeleo na amani , Umoja wa Mataifa umesema jumuiya ya kimataifa ya michezo inakabiliwa na changamoto kubwa wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 kwa watu wengi kushindwa kujumuika katika michezo mbalimbali na pia kufanya mazoezi. Flora Nducha na taarifa zaidi
(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mlipuko wa COVID-19 unasambaa kwa kasi katika nchi mbalimbali na hatua za kujitenga kuepuka mikusanyiko zimekuwa ndio maisha ya kila siku ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
Hatua hizo zimesababishwa vituo vya michezo, vituo vya kufanyia mazoezi, viwanja vya michezo, mabwawa ya umma ya kuogelea, vituo vya kujifunza muziki na maeneo ya watoto kwenda kucheza kufungwa..
 Na hii inamaanisha kwamba “wengi wetu hatuwezi kushiriki mazoezi ya viungo iwe mmoja mmoja au kwa vikundi vya michezo mbalimbali, au shughuli zozote za mazoezi ya viungo, wala kuangalia mashindano ya michezo moja kwa moja.” 
Umesema Umoja wa Mataifa ukiongeza kwamba na matokeo yake “jumuiya ya kimataifa ya michezo inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na hatua zilizochukuliwa na nchi mbalimbali kote duniani kupambana na COVID-19.”
Hata hivyo katika siku hii Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba hatua zote hizo hazimaanisi kwamba “sasa ndio tuache kufanya mazoezi ya viungo kabisa au tuache mawasiliano na makocha, wachezaji wenzetu, wakufunzi na mashabiki wenzetu wa michezo ambao sio tu kwamba wanatusaidia kuhakikisha tuko vyema kiviungo bali pia kijamii.”
Shirika la afya la umoja wa Mataifa WHO linapendekeza dakika 150 ya mazoezi ya wastani au dakika 75 za mazoezi makali kwa wiki au kufanya vyote. 
WHO imesema kuna njia mbalimbali za kuhakikisha watu wanajishuhulisha kiviungo wakati huu wa COVID-19 ikiwemo kutumia nyenzo za bure mtandaaoni na hivyo inawachagiza watu wa rika zote kuhakikisha wanafanya mazoezi ya aina moja au nyingine wakati huu mamilioni ya watu wakisalia majumbani.
Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa michezo ina uwezo wa kubadili dunia, ni haki ya msingi, nyenzo muhimu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuchagiza malengo ya maendeleo endelevu, amani, mshikamano na kuheshimiana.
Siku ya kimataifa ya michezo kwa ajili ya maendeleo na amani huadhimishwa kila mwaka Aprili 6.

 

 
===================================================
STUDIO: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
ASSUMPTA: 
Na sasa ni wakati wa makala ambapo msemaji wa serikali ya Kenya Cyrus Oguna anatoa ufafanuzi kuhusu nia ya tangazo la rais Uhuru Kenyatta la kutotoka wala kuingia katika baadhi ya miji. 
=================================================
STUDIO: PLAY MAKALA
====================================================

ASSUMPTA: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
ASSUMPTA:

Shukrani sana Jason Nyakundi kwa makala hii
====================================================
Na sasa ni  mashinani ambapo  ambapo mkuu wa Taasisi ya Global Change  Tony Blair anazungumzia jinsi wanashirikiana na UNESCO kusaidia wanafunzi kupata elimu wakati huu wa COVID-19.
 ===================================================
Studio: Play Mashinani
====================================================
ASSUMPTA:
Shukrani sana Tony Blair kwa ujumbe huo.
==================================================
STUDIO: Play Bridge

ASSUMPTA: Na hadi hapo natamatisha jarida letu la leo. Tupatane kesho kwa habari na makala kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa unaweza kupata matangazo na taarifa nyingine na kujifunza Kiswahili kwenye wavuti wetu news.un.org/sw. Msimamizi  wa matangazo ni FLORA NDUCHA na fundi mitambo na mimi ASSUMPTA MASSOI, nasema kwaheri kutoka New York.

==================================================
TAPE: CLOSING BAND

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
11'2"