Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kusalia majumbani kwa ajili ya kudhibiti COVID-19 kunazua hatari ya ukatili wa kijinsia-UN

Kusalia majumbani kwa ajili ya kudhibiti COVID-19 kunazua hatari ya ukatili wa kijinsia-UN

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka wito wa sitisho la ghasia na mapigano alilitoa hivi karibuni liguse pia ghasia zinazokumba wanawake na wasichana majumbani hususan wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19. Grace Kaneiya na ripoti kamili.
(Taarifa ya Grace Kaneiya)
Guterres amesema hayo katika tamko lake alilolitoa kwa serikali mbalimbali duniani wakati huu ambapo janga la COVID-19 pamoja na kusababisha machungu ya kiuchumi na kiuchumi, limeripotiwa kuleta machungu ndani ya nyumba sehemu mbalimbali duniani, wanawake wengi wakipiga simu za kusaka usaidizi.
(Sauti ya Antonio Guterres)
“Nilitoa wito kumaliza ghasia kila mahali, sasa. Lakini ghasia si katika uwanja wa vita pekee. Kwa wanawake wengi na wasichana, vitisho vimeshamiri pale ambapo panatakiwa pawe salama zaidi kwao. Majumbani mwao.Na hivyo natoa wito mpya leo hii kwa amani iwepo majumbani na katika nyumba, duniani kote.”

Amesema wito huo unatokana na ukweli kwamba, marufuku ya kusalia majumbanj na karantini pamoja na kuzuia  maambukizi ya COVID-19, yanaweza pia kufanya wanawake wawe kwenye mtego na wapenzi wao makatili.

Ni kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa serikali,zifanye huduma za kinga ya ukatili dhidi ya wanawake kuwa sehemu muhimu ya mikakati yao ya kitaifa ya kukabiliana na COVID-19, akimaanisha kwamba,
(Sauti ya Antonio Guterres)
“Ziongeze uwekezaji katika huduma za kusaka usaidizi kwa njia ya mtandao pia kuimarisha mashirika ya kiraia. Mifumo ya mahakama iendelee kushtaki wahalifu wa ukatili majumbani. Pia ziandae mifumo ya kutoa tahadhari kwenye maduka ya dawa na vyakula”
Halikadhalika ametaka serikali zitangaze kuwa makazi ya manusura ni huduma muhimu na ziweke njia salama kwa wanawake kusaka msaada bila ufahamu wa waliowatendea uovu akisema kuwa haki za wanawake na uhuru ni muhimu kujenga jamii thabiti na zenye mnepo.

Amekumbusha kuwa kwa pamoja dunia inapopambana ma COVID-19, inaweza na inapaswa kuzuia ukatili popote, kuanzia majumbani hadi uwanja wa vita.

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Grace Kaneiya
Sauti
2'9"
Photo Credit
UNMISS\Nektarios Markogiannis