Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano na tishio la COVID-19 lafurusha wakimbizi wa Burkina Faso-UNHCR

Mapigano na tishio la COVID-19 lafurusha wakimbizi wa Burkina Faso-UNHCR

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, bado lina hofu kubwa juu ya ongezekola ghasia nchini Burkina Faso, ghasia ambazo kila uchao zinafurusha watu kutoka kwenye makazi yao. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora Nducha)

UNHCR inasema kuwa kadri ghasia zinavyosambaa kwenye ukanda wa Sahel, Burkina Faso tangu mwezi Januari mwaka huu imeshuhudia zaidi ya watu 838,000 wakisalia wakimbizi wa ndani, idadi ambayo inazidi kuongezeka kila siku huku kuwasili kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, kukiongeza chumvi kwenye kidonda cha ukosefu wa usalama.

Msemaji wa UNHCR Babar Baloch akizungumza na waandishi wa habari kutokea Geneva, Uswisi kwa njia ya video amesema kuwa mashambulizi kutoka kwa wapiganaji waliojihami pia yameathiri wakimbizi 25,000 wa Mali ambao wanaishi kwenye kambi zilizo maeneo ya ndani zaidi karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso.

Amesema ghasia zimekumba majimbo 13 ya Burkina Faso ambapo wiki iliyopita watu wapatao 32 waliuawa katika mfululizo wa mashambulizi ilhali wengine kadhaa walijeruhiwa.

“Idadi kubwa ya wakimbizi hao sasa wameamua kurejea nyumbani licha ya ukosefu wa usalama huko nyumbani kwao wakiona kuwa ni bora zaidi kuliko ukimbizini,”  amesema Bwana Baloch akifafanua kuwa katika kambi ya Goudoubo ,iliyokuwa makazi ya wakimbizi 9,000, mashambulizi ya hivi karibuni yamesababisha isalie tupu kwa kuwa wakimbizi wa ndani wameamua kukimbia kusaka usalama kwingineko.

UNHCR imesema kuwa wakimbizi hao waliona kuwa kwa sababu shule zimefungwa, sambamba na kituo cha afya na kile cha usalama kwenye kambi yao, nusu ya wakazi wa kambi hiyo waliona bora wakimbie na nusu yao waliofikia maeneo ya Mopti, Gao na Timbuku walitaja ukosefu wa usalama kuwa sababu ya kurejea nyumbani kutoka Burkina Faso.

Nusu yao wamesaka hifadhi maeneo ya ndani mwa Burkina Faso ambapo takribani 2,500 wanaishi na wakimbizi wa ndani wa Burkina Faso kwenye mji wa Dori ambako nako mazingira ya maisha si mazuri na huduma kama vile maji safi, afya ni ngumu kupatikana.

Halikadhalika wakimbizi wengine nao wamesema wanataka kurejea nyumbani Mali pindi vikwazo vitokanavyo na virusi vya Corona vitakapolegezwa.

Hata hivyo msemaji huyo wa UNCHR amefafanua kuwa pamoja na hali ilivyo sasa wanashirikiana na mamlaka kupatia wakimbizi wanaorejea nyumbani makazi, vifaa vya misaada na fedha kusaidia maisha yao sambamba na vifaa vinavyohitajika kukabiliana na janga la COVID-19.

Audio Credit
Arnold Kayanda/Flora Nducha
Audio Duration
2'33"
Photo Credit
© UNICEF/Vincent Tremeau