Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu ukweli kuhusu COVID-19

Fahamu ukweli kuhusu COVID-19

Pakua

Tangu kuibuka kwa virusi vya corona, COVID-19, duniani kote watu wamekuwa nao wakiibua dhana mbalimbali potofu za kuhusu namna ya kujikinga au kutibu maambukizi ya virusi hivyo. Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, kupitia wavuti wake pamoja na mengine, limechapisha baadhi ya dhana hizo potofu na kuzitolea ufafanuzi kama anavyosimulia Flora Nducha


(Taarifa ya Flora Nducha )


WHO inasema wako watu walio na dhana kuwa kujianika katika jua kali au joto la kufikia nyuzi joto 25 kunaweza kuwazuia kupata virusi vya corona. Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linasisitiza kuwa dhana hiyo ni potofu kwani unaweza kupata virusi hivyo bila kujali kama umekaa juani muda mrefu au katika hali ya hewa yenye joto.

Bado WHO inasisitiza kuendelea kujilinda kwa kundelea kuosha mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa macho, mdomo na pua. 


Watu wengine wamekuwa wakiamini kuwa njia moja ya kujipima mwenyewe kama umeambukizwa virusi vya corona, COVID-19 ni kujaribu kubana pumzi bila kupumua kwa sekunde 10 au zaidi na kwamba usipokohoa au kujisikia vibaya basi hauna virusi vya corona. Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa linasema kuwa hiyo nayo ni dhana potofu kwani njia hiyo si tu haiwezi kukuthibitishia kuwa huna virusi vya corona, bali pia haiwezi kukweleza kuhusu magonjwa mengine ya mapafu. Kwa hivyo WHO inasisitiza njia bora ni kuangalia dalili za ugonjwa huu ambazo kikohozi kikavu, kuchoka na pia kuwa na homa. Ni vema kuwasiliana na wahudumu wa afya pindi unapoona una dalili za namna hiyo ili uweze kupatiwa msaada pamoja na kuwaepusha unaoweza kukutana nao.
 
Aidha WHO inasema wako watu wanaoamini kuwa unywaji wa pombe utawakinga na virusi vya corona, COVID-19, Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linawaambia watu hao kuwa pombe si tu haiwezi kukukinga na virusi hivyo, bali pia unywaji wa pombe wa mara kwa mara na uliopita kiwango, unaweza kuwa hatari na kukuweka katika matatizo ya kiafya. 
Na je kuoga maji moto kwaweza kukuepusha na virusi hivi vya corona? La hasha, kwa kawaida joto la mwili wa binadamu hubakia katika nyuzi joto 36.5 hadi nyuzi joto 37 bila kujali joto la maji anayoyaoga. Kimsingi, WHO wanakutahadharisha kuwa kuoga maji ya moto sana kunaweza kuwa hatari kwani unaweza kuunguza Ngozi yako. Kwa hivyo endelea kutumia njia zinazoshauriwa kitaalamu kama vile kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji tiririka. 


Vipi kuhusu Mbu? Kwani kuna wale wanaoamini kwamba huenda mbu anaweza kuwaambukiza virusi vya corona. Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linasema, hapana. Ingawa unapaswa kuwadhibiti mbu ili wasikuambukize magonjwa mengine kama vile malaria, hadi hivi sasa hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa wadudu hao wanaweza kusambaza virusi vya corona. Virusi vya corona, COVID-19 vinasambaa kwa pale ambapo maji maji kutoka kwa mtu aliyeathirika yanaposambaa na kuangukia mahali baada ya kupiga chafya au kukohoa au maji maji mengine kutoka mdomoni na katika pua. 
 
Vilevile wapo wale wenye imani kuwa ulaji wa vitunguu saumu kunaweza kuwakinga na COVID-19. WHO inaeleza kuwa ijapokuwa vitunguu saumu ni chakula cha afya lakini hakuna ushahidi wowote kuwa kinaweza kukusaidia kuzuia kuambukizwa virusi vya corona. Kwa hivyo endelea kuwasikiliza wataalamu wa afya

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Flora Nducha
Audio Duration
3'34"
Photo Credit
UN News/Elizabeth Scaffidi