Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

31 Machi 2020

31 Machi 2020

Pakua

Assumpta Massoi : Hujambo na Karibu kusikiliza Jarida kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, kutoka hapa New York Marekani.

JINGLE (04”)      

ASSUMPTA:Ni Jumanne ya Machi 31 mwaka 2020, mwenyeji wako studioni hii leo ni mimi ASSUMPTA MASSOI 

1: Uganda yapitisha amri ya kutotembea usiku kudhibiti COVID-19
Uganda imefuata nyayo ya baadhi ya nchi duniani ya kupitisha amri ya kutotembea usiku kama mojawapo ya njia za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, sanjari na kufunga mipaka yake na kupiga marufuku usafiri wa magari binafsi. Haya hapa  maelezo zaidi na mwandishi wetu wa Uganda, John Kibego.
(Taarifa ya John Kibego)
Rais Yoweri Kaguta Museveni ametangaza maagizo mapya mapya kabisa kwa madhumuni ya kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi hivyo nchini Uganda.
Amri kubwa zaidi ni zile sheria ya kutotembea usiku isipokuwa magari ya mzigo, kubana mikutano ya watu zaidi ya watano kutoka 10 waliokuwawamekubaliwa katika maagizo ya kwanza, kuagizawa kwa wahudumu wa umma kusalia majumani ila wale wale wanohusika na vita dhidi ya COVDI-19 ikiwemo waugizi na waganga wa mifugo,  askari na wafanyakazi wa makambuni yanayotoa huduma za maji na umeme.
 Kulingana na Raisi Museveni, maagizo 16 ya ziada yametolewa kutokana na wanchi kutotii maagiszo ya kwanza kama ilivyotarajiwa kiasi kwamba magari binafsi yaligeuzwa kuwa ya abiria kisiri na kusawazisha malengo ya kubana usafiri wa umma.
(Sauti ya Museveni)
“Magari binafsi yalikuwa yamegeuzwa kuwa vyombo vipya vya usafiri wa umma bila leseni huku wakiongeza uwezekano wa maambukizo. Marufuku dhidi ya usafiri binafsi uliokuwa umegeuzwa kuwa wa abiria inaanza kutekelezwa saa nne za usiku wa leo. Kuanzia saa moja ya usiku wa tarehe 31 Machi hamna kutembea usiku kote nchini na maduka yote yasio ya chakula ni lazima yafungwe”
Magari yote ya serikali yataegeshwa kwenye  makao makuu ya serikali za mitaa na madereva wao tayari kuitikia dharura yoyote kuhusu COVID-19, kwa usimamizi wa kamati mahsusi za kupambana na virusi hivyo.
Masoko ya chakula yataendelea na kazi endapo tu mamlaka zao za usimamizi zitahakikisha kwamba wachuruzi hawarejei majumbani hadi mwisho wa siku 14 za maagizo haya mapya na kutii maagizo yote wizara ya afya kuhusiana na COVID-19.
Amewashauri kujenga mahema nje ya masoko husika kuliko kurejea majumbani kila jioni kinachohatarisha familia na jamii zao. Kutokwenda nyumbani kila siku pia kunahusu wafanyakazi wa viwandani na makampuni ya ujenzi wanaotaka kuendelea na akzi wakati huu wa tahadhari ya COVID-19.

===================================================

2: COVID-19 ni msumari wa moto juu ya kidonda kwa watoto DRC:UNICEF 
 
Mfumo wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, unahitaji msaada wa haraka wakati huu ukilemewa na magonjwa ya surua na kipindupindu yanayokatili maisha ya maelfu ya watoto pamoja na tishio la janga jipya la virusi vya Corona COVID-19. Jason Nyakundi na maelezo zaidi.
 
(TAARIFA YA JASON NYAKUNDI)
 
Janga hilo ni dhahiri na miongoni mwa waliokumbwa nalo ni Mama Bwanga mkazi wa eneo la Mikonga kwenye viunga vya Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Alikuwa na watoto watano lakini wawili wao walifariki dunia kutokana na surua, mmoja alifariki na umri wa miaka minne na mwingine mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu alifariki dunia wiki moja baadaye, na anasema,
(Sauti ya Mama Bwanga)
“Kwanza alikuwa na vipele mwili mzima, kisha macho yake yalikuwa mekundu, alikuwa hawezi kula. Walimpatia dawa lakini hakupata nafuu, alifariki dunia na umri wa miaka minne. Mtoto wa pili alikufa wiki moja baadaye, naye pia Jumanne. Ili kusahau machungu, nazungumza na watu lakini majonzi yanarejea, nalia. Tulikosa fedha na taarifa kuhusu chanjo ya surua.”
Sasa kumbukizi yake ni picha tu ambapo UNICEF katika ripoti yake ya leo kuhusu surua na kipindupindu DRC inasema kwamba, juhudi za kukabiliana na Ebola Mashariki mwa nchi hiyo zimebadili mtazamo na kupeleka rasilimali katika janga hilo kutoka kwenye vituo vingine vya afya ambavyo tayari vimezidiwa kwa kukabiliana na magonjwa mengi ya mlipuko.
 
Tangu mwanzo wa mwaka 2019 mlipuko wa surua ambao ni mbaya zaidi kushuhudiwa duniani umekatili maisha ya watoto zaidi ya 5,300 wenye umri wa chini ya miaka mitano huku pia kukiwa na wagonjwa 31,000 wa kipindupindu.
 
Kana kwamba maradhi hayo hayatoshi ripoti inasema "sasa mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 unasambaa kwa kasi na kutoa mtihani mkubwa kwa nchi hiyo ambayo imeelezwa kuwa katika hatari zaidi barani Afrika.”
UNICEF imeongeza kuwa hali hii ni sawa na kuweka msumari wa moto juu ya kidonda kwani katika vituo vya afya vya umma, vifaa, wahudumu wenye ujuzi na fedha ni haba. Vituo vingi vinakosa hata huduma za msingi za maji na usafi na kiwango cha chanjo ambacho kilikuwa chini sasa kimeshuka zaidi kwa mwaka mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNICEF takriban watoto milioni 3.3 nchini DRC wanakosa huduma za msingi za afya, huku katika nchi nzima watoto milioni 9.1 karibu mtoto 1 kati ya 5 waliochini ya miaka 18 anahitaji msaada wa kibinadamu.
UNICEF imeonya kwamba "endapo vituo vya afya havitapata njia ya kufikisha chanjo, lishe na huduma zingine za msingi ikiwemo kwenye maeneo ya vijijini nchini humo basi tuna hatari ya kushuhudia maisha na mustakabali wa watoto wengi wa Congo ukisambaratishwa na magonjwa yanayoweza kuzuilika."
====================================================
STUDIO. MIDWAYSTING
====================================================
ASSUMPTA: Na punde ni makala na leo tunakwenda nchini Tanzania kuangazia jinsi kampuni binafsi zinavyounga mkono harakati za kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona nchini humo, usibanduke.
====================================================

3: COVID-19 yasababisha Olimpiki kusogezwa mwaka mmoja mbele, sasa kuchezwa 2021 
Takribani siku 20 tangu Mwenge wa Olimpiki kukabidhiwa kwa mji mwenyeji wa michezo ya mwaka huu wa 2020, Tokyo, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC imetangaza  kuisogeza michuano hiyo mwakani ili kupisha mapambano dhidi ya virusi vya corona, COVID-19. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace Kaneiya)
 
Tangazo hili la kusogeza michezo hii ya Olimpiki ambayo ilikuwa ifanyike mwaka huu mjini Tokyo Japan, limekuja takribani wiki moja baada ya kutangazwa kuahirishwa kwa michezo hiyo huku tayari mwenge wa Olimpiki ukiwa unaiangazia dunia katika mikono ya mchi wenyeji Japan. Siku ishirini tu tangu Mwenge huo ulipokabidhiwa kwa nchi wenyeji. 
 
Mamlaka za Olimpiki pamoja na za Japan zimetangaza kuwa sasa michezo hiyo inayowakutanisha washiriki wa michezo mbalimbali kutoka kote duniani kuwa itafanyika kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 8 Agosti mwakani, ikifuatiwa na ile ya watu wenye ulemavu itakayofanyika kuanzia tarehe 24 Agosti hadi tarehe 5 Septemba 2021.
 
Tarehe hizo mpya zilizopangwa mwaka mmoja kamili tangu tarehe ambazo zilikuwa zimepangwa awali ambapo michezo hiyo ingefanyika mwaka huu wa 2020.
Thomas Bach, Rais wa Kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC anasema, 
 
(Sauti ya Thomas Bach)
 
“hii leo tumeweka tarehe za michezo ya Olimpiki yam waka huu 2020 mjini Tokyo kuwa zitafanyika mwaka ujao wa 2021. Kwa michezo ya Olimpiki, kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 8 Agosti na michezo ya Paralimpiki kuanziatarehe 24 mwezi Agosti hadi tarehe 5 mwezi Septemba.”
 
Bwana Bach, anaongeza kusema,
 
(Sauti ya Thomas Bach)
 
“tulichagua tarehe hizi kufuata kanuni zetu, ambazo tulizianzisha tarehe 17 Machi, na hii ni, kwanza kabisa, kulinda afya ya mtu yeyote anayehusika katika Michezo ya Olimpiki na kutoa mchango wetu katika kuvidhibiti virusi - ukweli ambao umekubaliwa, miongoni mwa wengine wengi, pia na mkutano mkuu wa G20 hivi karibuni. Na tulilazimika kuangalia katika kalenda ya michezo ya kimataifa ili kudumisha umoja wa Michezo ya Olimpiki. Pamoja na sababu hizi, sasa tunaweza kutarajia kuwa na Michezo hii msimu ujao wa kiangazi, ambao ni kipindi ambacho pia kinaweza kusimamiwa na wadau wetu wajapan na marafiki kwa sababu mara zote walisema tarehe katika msimu wa joto wa mwaka 2021.”
 
Taarifa ya awali ya OIC imesema kuwa wanamichezo wote ambao tayari walikuwa wamefuzu na tayari wamepangiwa kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020 hawatabadilishwa aingawa hivi sasa changamoto zitakuwa nyingi ikiwemo namna ya kushughulika na vyombo vya habari ambavyo vilikuwa tayari kupeperusha michezo hiyo na pia wadhamini ambao walikuwa tayari wamejiandaa kwa ajili ya mwaka huu. 
 
Hata hivyo imetangazwa kuwa mwenge wa Olimpiki ambao tayari ulikuwa umewasili nchini Japan tangu tarehe 20 ya mwezi huu wa Machi, utaendelea kuwaka kwa mwaka mzima hadi michuano hii itakapochezwa mwakani. 
===================================================
STUDIO: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
ASSUMPTA:  Na sasa ni makala ambapo Ahimidiwe Olotu, kutoka kituo cha habari za Umoja wa Mataifa, UNIC, jijini Dar es salaam, nchini Tanzania anazungumza na Jestina George-Meru,Mkurugenzi wa kampununi ya Zuri Africa, kuhusu harakati zao za kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona nchini humo.
=================================================
STUDIO: PLAY MAKALA
==================================================== 

ASSUMPTA: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
ASSUMPTA:  

Shukrani sana Ahimidiwe Olotu kwa makala hiyo.
====================================================
Na sasa ni  mashinani ambapo msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Rupert Colville anatoa wito wa kuwalinda wazee dhidi ya janga la virusi vya Corona.
====================================================
Studio: Play Mashinani
====================================================
ASSUMPTA: 
Asante sana  Rupert Colville kwa ujumbe huo.
==================================================
STUDIO: Play Bridge

ASSUMPTA: Na hadi hapo natamatisha jarida letu la leo. Tupatane kesho kwa habari na makala kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa unaweza kupata matangazo na taarifa nyingine na kujifunza Kiswahili kwenye wavuti wetu news.un.org/sw. Msimamizi  wa matangazo ni FLORA NDUCHA na fundi mitambo na mimi ASSUMPTA MASSOI, nasema kwaheri kutoka New York. 

==================================================
TAPE: CLOSING BAND

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
12'33"