Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO na UNICEF yatoa mapendekezo ya namna ya waajiri kusaidi familia waajiriwa na familia zao

ILO na UNICEF yatoa mapendekezo ya namna ya waajiri kusaidi familia waajiriwa na familia zao

Pakua

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la kazi, ILO leo wametoa mapendekezo ya jinsi waajiri wanaweza kusaidia waajiriwa na familia zao wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19. Flora Nducha na ripoti kamili.
(Taarifa ya Flora Nducha)
Taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo mjini New York, Marekani imesema kadri gonjwa hilo linavyozidi kusambaa, ni muhimu kusaidia familia kupunguza madhara yake kwa watoto wakisema kuwa, “kupoteza ajira, shule kufungwa na ukosefu wa huduma za malezi ya watoto kunamaanisha kwamba familia hasa zile zenye kipato cha chini zinahitaji msaada za ziada.”
 
Mkuu wa masuala ya uendelezaji watoto, UNICEF, Dkt. Pia Rebello Britto amesema kuwa, “Madhara ya COVID-19 ikiwemo kupoteza ajira, msongo wa kupitiliza na kudorora kwa afya ya akili kutagusa familia nyingi katika miaka ijayo. Kwa watoto wengi walio hatarini, ukosefu wa mifumo ya kutosha ya hifadhi ya jamii kunaongeza hatari ya wao kutumbukia zaidi kwenye madhara hayo.”
 
UNICEF na ILO wanatoa wito kwa serikali kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii hususan kwa familia maskini ikiwemo kusaidia waajiriwa kuendelea na ajira na kupata kipato na kuwapatia hakikisho la usaidizi wa kifedha wale ambao wanapoteza ajira zao.
Mkurugenzi wa ILO kuhusu mazingira ya kazi Manuela Tomei anasema wao wanasisitizia mashauriano na ushirikiano baina ya serikali, wafanyakazi na waajiri pamoja na wawakilishi wa waajiriwa.
Mathalani, sera na vitendo ambavyo ni rafiki kwa familia kama vile ulinzi wa ajira za wafanyakazi na vipato vyao, likizo yenye malipo kwa ajili ya kuuguza au kutunza familia, saa za kazi ziendanazo na mahitaji ya mwajiriwa na kupata huduma bora ya malezi ya watoto.
Ni kwa kuzingatia msingi huo, mapendekezo ya mashirika hayo mawili ni pamoja na kufuatilia na kufuata ushauri wa mamlaka za kitaifa na kieneo na kusambaza taarifa hizo kwa wafanyakazi.
Pia kutathmni iwapo sera za sasa za pahala pa kazi zinatoa usaidizi wa kutosha kwa wafanyakazi na familia zao.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi /Flora Nducha
Audio Duration
2'6"
Photo Credit
Man Yi