Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ITU na UNESCO washirikiana kuhakikisha elimu kwa wanafunzi

ITU na UNESCO washirikiana kuhakikisha elimu kwa wanafunzi

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO limezindua muungano wa elimu wa kimataifa ili kuhakikisha wanafunzi walio nje ya shule kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 wanasoma kupitia teknolojia. John Kibego na taarifa zaidi

(TAARIFA YA JOHN KIBEGO)

Akizungumzia umuhimu wa kuzinduliwa kwa muungano huo mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema hadi kufikia Machi 25  wiki hii wanafunzi zaidi ya wanafunzi bilioni 1.4 wa shule na vyuo kote duniani wameshindwa kuhuduria masomo kutokana na janga la COVID-19 na ndio maana UNESCO imeamua kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha watu hao wanapata elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo kutumia teknolojia . Hata hivyo Bi Azoulay ameongeza kuwa

(SAUTI YA AUDREY AZOULAY)

“Mwanzo hauko sawa kwa kila mtu na hatari kubwa ni kwamba watoto kutoka katika jamii zisizojiweza watakosa elimu, na hatuwezi kuruhusu hili kutokea. Ukubwa wa changamoto hii unahitaji ubunifu, ushirikiano, na mshikamano tunahitaji kuchukua hatua haraka na kufanyakazi kama kitu kimoja. Na hii ndio sababu UNESCO inazindua muungano wa kimataifa wa elimu leo hii.”

Ameongeza kuwa miongoni mwa wadau ni pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia, makampuni ya habari na watalaam wa teknolojia ili kusaidia kufanikisha azma hii. Miongoni mwa wadau hao ni shirika la kimataifa la muungano wa mawasiliano ITU linaloongozwa na Katibu Mkuu Houlin Zhao

(SAUTI YA HOULIN ZHAO- )

“Shirika letu ITU limejizatiti kuunganisha watu wote duniani, popote waliko na kwa njia yoyote. Kupitia kazi yetu tunalinda na kuunga mkono haki ya kila mtu kuwasiliana. Katika wakati huu wa janga tumedhamiria kushirikiana na UNESCO na wajumbe wengine kuhakikisha muendelezo wa elimu majumbani kutumia radio, televisheni, brodibandi, 4G, 5G,  na teknolojia ya intaneti.

UNESCO inasema inaamini kwa kwa pamoja kupitia muungano huu mpya wa kimataifa wa elimu utaweza kuzisaidia nchi kuja na suluhu mpya za kufikisha elimu kwa mamilioni ya wanafunzi na kuhakikisha hakuna anayesalia nyuma.

Audio Credit
Arnold Kayanda/ John Kibego
Audio Duration
2'14"
Photo Credit
UN Photo/Manuel Elías