Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi latolewa kwa ajili ya nchi masikini kukabili virusi vya corona

Ombi latolewa kwa ajili ya nchi masikini kukabili virusi vya corona

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amezindua ombi la dola bilioni 2 ili kusaidia harakati za kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 katika nchi maskini zaidi duniani. Flora Nducha na ripoti kamili.
 
(Taarifa ya Flora Nducha)
 
Uzinduzi huo umefanyika jijini New York, Marekani kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya video wakati huu ambapo hadi leo hii katika nchi 195 zenye maambukizi kuna jumla ya wagonjwa 375,498 wa virusi vya Corona na watu 16, 362 wamefariki dunia.
 
Akihutubia mkutano ulioleta wadau nao kwa njia ya video wakiwemo wakuu wa mashirika ya  Umoja wa Mataifa ya afya, WHO, kuhudumia watoto, UNICEF na misaada ya dharura, OCHA, Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amesema nchi hizo maskini zaidi duniani ni zile ambako mifumo ya afya ni dhaifu na zinahifadhi watu waliofurushwa makwao kwa sababu ya mabomu, ghasia, mafuriko, wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa karatasi za plastiki au wamelundikana kwenye kambi za wakimbizi au makazi yasiyo rasmi.
“Watu hawa hawana nyumba au makazi ambamo kwamo wanaweza kujitenga na wengine ili kuepusha maambukizi ya virusi vya Corona,”  amesema Guterres.
Fedha zitatumika kupeleka vifaa muhimu vya maabara kwa ajili ya kupima virusi vya Corona, na vifaa vya matibabu kwa wagonjwa wa COVID-19, kuweka vituo vya kunawa mikono kwenye kambi na makazi ya wakimbizi, kuzindua kampeni za uelimishaji kuhusu jinsi ya kujilinda na kulinda wengine dhidi ya virusi vya Corona na Kuanzisha vituo vya safari za ndege barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini ili kusafirisha wahudumu wa kibinadamu na vifaa kule kwenye mahitaji zaidi.
 
Amekumbusha kuwa, “iwapo fedha hizo zitatumika ndivyo sivyo, basi itakuwa ni janga “kipindupindu kitasambaa, surua na homa ya uti wa mgongo. Viwango vya utapiamlo vitaongezeka, na hivyo kufutilia mbali uwezo wa mataifa hayo kukabiliana na virusi vya Corona.”
 
Ni kwa mantiki hiyo amesema fedha zinazoombwa zitaratibiwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura na majanga, OCHA, na fungu hilo linajumuisha maombi mapya pamoja na ya awali yaliyokwishatangazwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na wadau wake na Katibu Mkuu ameomba mataifa na wahisani wachangie kwa kuwa ni jambo la kimaadili na maslahi kwa dunia nzima.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Flora Nducha
Audio Duration
2'31"
Photo Credit
UN Kenya/Newton Kanhema