Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

25 Machi 2020

25 Machi 2020

Pakua

Assumpta Massoi : Hujambo na Karibu kusikiliza Jarida kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, kutoka hapa New York Marekani.

JINGLE (04”)      

ASSUMPTA:Ni Jumatano ya Machi 25 mwaka 2020, mwenyeji wako studioni hii leo ni mimi ASSUMPTA MASSOI 

1: UN yazindua ombi la dola bilioni 2 kusadia nchi maskini kukabili virusi vya Corona
 
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amezindua ombi la dola bilioni 2 ili kusaidia harakati za kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 katika nchi maskini zaidi duniani. Flora Nducha na ripoti kamili.
 
(Taarifa ya Flora Nducha)
 
Uzinduzi huo umefanyika jijini New York, Marekani kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya video wakati huu ambapo hadi leo hii katika nchi 195 zenye maambukizi kuna jumla ya wagonjwa 375,498 wa virusi vya Corona na watu 16, 362 wamefariki dunia.
 
Akihutubia mkutano ulioleta wadau nao kwa njia ya video wakiwemo wakuu wa mashirika ya  Umoja wa Mataifa ya afya, WHO, kuhudumia watoto, UNICEF na misaada ya dharura, OCHA, Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amesema nchi hizo maskini zaidi duniani ni zile ambako mifumo ya afya ni dhaifu na zinahifadhi watu waliofurushwa makwao kwa sababu ya mabomu, ghasia, mafuriko, wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa karatasi za plastiki au wamelundikana kwenye kambi za wakimbizi au makazi yasiyo rasmi.
“Watu hawa hawana nyumba au makazi ambamo kwamo wanaweza kujitenga na wengine ili kuepusha maambukizi ya virusi vya Corona,”  amesema Guterres.
Fedha zitatumika kupeleka vifaa muhimu vya maabara kwa ajili ya kupima virusi vya Corona, na vifaa vya matibabu kwa wagonjwa wa COVID-19, kuweka vituo vya kunawa mikono kwenye kambi na makazi ya wakimbizi, kuzindua kampeni za uelimishaji kuhusu jinsi ya kujilinda na kulinda wengine dhidi ya virusi vya Corona na Kuanzisha vituo vya safari za ndege barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini ili kusafirisha wahudumu wa kibinadamu na vifaa kule kwenye mahitaji zaidi.
 
Amekumbusha kuwa, “iwapo fedha hizo zitatumika ndivyo sivyo, basi itakuwa ni janga “kipindupindu kitasambaa, surua na homa ya uti wa mgongo. Viwango vya utapiamlo vitaongezeka, na hivyo kufutilia mbali uwezo wa mataifa hayo kukabiliana na virusi vya Corona.”
 
Ni kwa mantiki hiyo amesema fedha zinazoombwa zitaratibiwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura na majanga, OCHA, na fungu hilo linajumuisha maombi mapya pamoja na ya awali yaliyokwishatangazwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na wadau wake na Katibu Mkuu ameomba mataifa na wahisani wachangie kwa kuwa ni jambo la kimaadili na maslahi kwa dunia nzima.

===================================================

2: COVID-19: Uganda yapiga marufuku wakimbizi kuingia nchini humo
 
Serikali ya Uganda imesema kutokana na kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, wakimbizi hivi sasa hawataingia nchini humo huku ikizuia hata huduma za kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo zilizokuwa zikitolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwenye vituo vya mapokezi ya wakimbizi. John Kibego na ripoti kamili kutoka Uganda.
 
 
 (Taarifa ya John Kibego)
Taarifa iliotolewa leo kuhusu msimamo wa serikali kwa wakimbizi wanaopitia migogoro isiojali mlipuko wa COVID-19 duniani, Musa Ecweru naibu waziri wa wakimbizi na kushughulikia majanga ametangaza rasmi kuwa kamwe kamwe wasakahifadhi hawataruhusiwa tena kukanyaga kwenye ardhi ya Uganda.
Amesema hayo saa chache baada ya kuthibitishwa kwa wagonjwa watano zaidi wa COVID-19 kando na tisa waliothibitishwa kwanzia usiku w aJumamosi wiki iliopita.
Hivyo Bwana Ecweru amesema hawawezi tena kuvumilia wakimbizi zaidi kuingia au kukaa nchini Uganda na kwa kutekeleza azimio hilo, wameanza kufunga mapokezi yote ya wakimbizi mpakani na mpakani na kisha kupunguza idadi ya waliokuwa tayari kwenye mapokezi ya wakimbizi makambini.
Akiongea akiwa mkali bwana Ecweru amesema si kw akuchukia wakimbizi lakini ni kwa kuhakikisha usalama wa Waganda na majirani zake.
Umauzi huo pia umetangazwa rasmi wakati ambapo wakimbizi 20 kutoka Jmahuri ya Kidemokrasia ya Kongo, (DRC) wameweka chini ya karantini ya siku 14 kuchunguzwa hali yao ya virusi vya COVID-19 wakiwa kwenye ufukwe wa Ziwa Albert wilayani Kagadi
Askari mmoja wa mpakani aliyetuhumiwa kuwatorosha kuingia nchini baada ya mpaka kufungwa amekamatwa na polisi.
Duniya Aslam Kahan Msemaji wa UNHCR, Uganda amesema kufuatia uamuzi huo, wameanza kuhamisha kwa dharura wasakahifadhi waliokuwa kwenye mapokezi ya wakimbizi kadi makambini.
Hata hivyo amesema msimamo wa UNHCR ni kuyaomba mataifa kuhakikisha wanatii haki za wakimbizi na makundi mengine yaliohatarini kwa kupunguz avikwazo mipakani na kuzingatia uhuru wa kutembea.
Wagonjwa wapya watano waliothibitishwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya Henry Mwebesa ni raia wa Uganda watatu akiwemo mtoto mchanga mwneye umri wa miezi minane na Wachina wawili walioingia nchini wiki iliopita.

====================================================
STUDIO. MIDWAYSTING
====================================================
ASSUMPTA: Na punde ni makala ambapo leo tutakuwa Mkoani Geita, Tanzania kusikia maoni ya wananchi kuhusu virusi vya corona au COVID-19.
====================================================

3: Mradi wa pamoja wa UN-Habitat ni msaada kwa wakazi wa mtaa wa Mathare, Kenya
Shirika la makazi la Umoja wa Mataifa, UN-Habitat kwa kushirikiana na kituo cha mazingira cha vijana eneo la Mathare jijini Nairobi, Kenya, au  Mathare Environmental One Stop Youth Centre wameungana kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi ya kunawa mikono kwa wakazi 50,000 wa kijiji cha Mlango Kubwa katika mtaa wa Mathare ulioko kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.
(Taarifa ya Grace)
Video ya UN-Habitat inaonesha wakazi wa Kijiji cha Mlango Kubwa kwenye mtaa wa Mathare katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, wakiendelea na shughuli za kila siku. 
Msongamano wa watu na ukosefu wa maji ya kujisafi huenda vikahatarisha wakazi wa mitaa duni kuambukizwa virusi vya corona.
Lakini maradi huu wa pamoja ni  hatua ya kulinda watu hao ambao kwa kawaida husaka maji kwenye maeneo ya umma. Maji hayo yanasafirishwa kwa kutumia mikokoteni yakiwa kwenye mitungi ya plastiki.
Kituo hiki kwa ushirikiano na UN-Habitat ni cha kwanza cha aina hiyo kwa ajili ya kunawa mikono  ambapo mradi huo unatarajiwa kuanzishwa katika maeneo mengine ya mitaa ya mabanda ya Mathare.
Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni ni moja ya mapendekezo a wataalamu wa afya kama moja wapo ya hatua za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.
Hatua hii inakuja wakati huu ambapo hadi Jumanne wiki hii Kenya imeripoti wagonjwa 25 wa virusi vya corona, COVID-19 waliothibitishwa.


===================================================
STUDIO: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
ASSUMPTA:  Na sasa ni wasaa wa makala ambapo Baraka Fulgence wa Redio washirika Storm FM amepita katika mitaa ya mji wa Geita kusikia maoni ya wananchi kuhusu COVID-19 au virusi vya corona namna wanavyouelewa ugonjwa huo.
=================================================
STUDIO: PLAY MAKALA
==================================================== 

ASSUMPTA: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
ASSUMPTA:  

Shukrani Baraka Fulgence kwa makala hiyo.

====================================================
Na sasa ni  mashinani tuungane na Mark Lowcock  Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura, OCHA akizungumzia mwongozo wa kuendelea kusambaza misaada ya dharura ya kibinadamu wakati huu wa janga la COVID-19.
====================================================
Studio: Play Mashinani
====================================================
ASSUMPTA: 
Asante sana Mark Lowcock ujumbe huo.
==================================================
STUDIO: Play Bridge
ASSUMPTA: Na hadi hapo natamatisha jarida letu la leo. Hadi wakati mwingine kwa habari na makala kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa unaweza kupata matangazo na taarifa nyingine na kujifunza Kiswahili kwenye wavuti wetu news.un.org/sw. Msimamizi  wa matangazo ni FLORA NDUCHA na fundi mitambo na mimi ASSUMPTA MASSOI, nasema kwaheri kutoka New York. 

==================================================
TAPE: CLOSING BAND

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
11'29"